• Nairobi
  • Last Updated May 4th, 2024 5:55 AM
NI KISASI: Atletico kwenye mizani ya Juventus huku City ikialika Shalke UEFA

NI KISASI: Atletico kwenye mizani ya Juventus huku City ikialika Shalke UEFA

TURIN, ITALIA

JUVENTUS watakuwa leo Jumanne wenyeji wa Atletico Madrid katika mchuano wa mkondo wa pili wa mwondoano wa Klabu Bingwa Ulaya (Uefa).

Katika mechi nyingine, Manchester City watawaalika Schalke kutoka Ujerumani uwanjani Etihad. Juventus wana ulazima wa kusajili ushindi wa zaidi ya mabao mawili ili kuweka hai matumaini ya kusonga mbele katika kampeni za kipute hicho muhula huu.

Chini ya kocha Diego Simeone, Atletico ambao walikuwa wanafainali wa 2015-16 waliwakwaruza Juventus 2-0 katika mchuano wa mkondo wa kwanza uliopigiwa ugani Wanda Metropolitano mnamo Februari 20.

Hata hivyo, mkufunzi Massimiliano Allegri anatazamiwa kutegemea zaidi maarifa ya nyota Cristiano Ronaldo ambaye atashirikiana vilivyo na Mario Mandzukic, Paulo Dybala, Juan Cuadrado, na Douglas Costa katika idara ya mbele.

Man-City watashuka dimbani wakijivunia ushindi wa 3-2 waliovuniwa katika mkondo wa kwanza kupitia kwa mabao ya mafowadi Leroy Sane na Raheem Sterling.

Ingawa miamba hawa wa soka ya Uingereza wanapigiwa upatu wa kuwapepeta Schalke kirahisi, mkufunzi wao Pep Guardiola amewataka kujihadhari zaidi.

Kulingana na Guardiola, Schalke hutawaliwa na hamasa tele zaidi kila wanapocheza ugenini na hapana shaka kwamba azma yao katika mchuano wa leo ni kuyazima makali yao ugani Etihad.

“Wana sifa sawa na Man-United na Ajax ambao walifufuka ugenini na kuwaduwaza wengi walipowachabanga PSG na Real Madrid mtawalia,” akasema.

Ushindi kwa Man-City utaweka hai matumaini yao ya kujitwalia jumla ya mataji manne katika kampeni za msimu huu.

Mbali na ufalme wa Uefa, Man-City wanafukuzia pia ubingwa wa Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) na Kombe la FA.

Taji la Carabao

Kikosi hicho tayari kimetia kibindoni taji la Carabao Cup baada ya kuwapepeta Chelsea katika fainali iliyowakutanisha mwishoni mwa mwezi jana.

Mchuano wa leo Jumanne utampa Guardiola jukwaa mwafaka la kumwajibisha beki John Stones ambaye atalijaza pengo la Nicolas Otamendi aliyeonyeshwa kadi nyekundu katika mechi ya raundi ya kwanza iliyochezewa ugani Veltins Arena.

Mbali na kuzikosa huduma za Otamendi, Man-City watalazimika kuyakosa maarifa ya Kevin De Bruyne, Fernandinho, Benjamin Mendy na Claudio Bravo wanaouguza majeraha mbalimbali.

Kwa upande wao, Schalke watakuwa bila ya wachezaji Alessandro Schopf, Omar Mascarell na Daniel Caligiuri ambao watasalia mkekani kwa kipindi kirefu zaidi kuuguza majeraha.

Miamba hao wa soka ya Ujerumani wanatarajiwa kumdumisha kipa Ralf Fahrmann michumani huku mlinda-lango mzoefu Alexander Nubel akisalia benchi.

Licha ya mchuano wa mkondo wa kwanza kutawaliwa na wingi wa hisia kali zilizochangia penalti na kadi nyekundu, Man-City walitamba na hivyo kusajili ushindi wao wa tatu katika jumla ya mechi nne za awali dhidi ya Schalke.

Ushindi wa pekee uliowahi kusajiliwa na Schalke dhidi ya Man-City ni katika nusu-fainali ya Cup Winners Cup iliyowakutanisha mnamo 1970.

Ingawa hivyo, wameshindwa kuwafunga wapinzani wao hao mara moja pekee katika matokeo ya 2-0 kwenye Ligi ya Uropa mnamo 2008.

Man-City wanajibwaga katika mchuano wa leo wakijivunia hamasa tele kutokana na ufanisi wa kusajili ushindi katika jumla ya mechi tisa zilizopita kwenye mapambano yote.

Mechi yao ya mwisho ilimalizika kwa wao kujivunia ushindi wa 3-1 dhidi ya Watford katika EPL uwanjani Etihad.

Kinyume na wenyeji wao, Schalke wamepoteza jumla ya michuano minne kwa mpigo katika Ligi Kuu ya Ujerumani (Bundesliga) tangu wazidiwe maarifa na Man-City.

Kesho Jumatano itakuwa zamu ya Bayern Munich kuwaalika Liverpool nchini Ujerumani huku Olympique Lyon ya Ufaransa ikiwaendea Barcelona uwanjani Camp Nou, Uhispania.

Ratiba ya UEFA (Leo Jumanne):

Manchester City na Schalke

Juventus na Atletico

(Kesho Jumatano):

Bayern na Liverpool

Barcelona na Lyon

You can share this post!

K’Ogalo yasukumwa hadi mkiani Zamalek ikipepea

Arsenal yazima makali ya United kutua nne-bora EPL

adminleo