Michezo

Nigeria, Algeria katika gozi la nguo kuchanika

July 13th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na MASHIRIKA

CAIRO, Misri

Baada ya kuwabandua Ivory Coast 4-3 kupitia kwa mikwaju ya penalti Alhamisi usiku, Algeria wanaopigiwa upatu wa kutwaa taji la mwaka huu watakutana na Nigeria kesho Jumapili katika nusu-fainali, kuanzia saa nne usiku.

Nusu-fainali ya kwanza itakutanisha timu za Senegal na Tunisia kuanzia saa mbili usiku.

Baghdad Bounedjah aliifungia Algeria bao katika muda wa kawaida kabla ya Johanthan Kodjia kusawazishia Ivory Coast.

Wakati wa penalti, Youcef Belaili wa Algeria alipoteza penalti yake kwa kupiga mwamba wa goli, sawa na Serey Die wa Ivory Coast.

Bounedjah alikuwa amepoteza penalti awali katika muda wa kawaida na kuwapa wasiwasi mashabiki wa timu yake ambao wamesubiri ubingwa wa taji hili tangu waunyakue kwa mara ya mwisho mnamo 2010.

Ni mechi ambayo Ivory Coast walitawala kwa kiasi kikubwa hasa katika kipindi cha kwanza, huku kipa Rais Mbolhi akikumbwa na wakati mgumu wa kupangua makombora ya washambuliaji wa timu hiyo kutoka Afrika Magharibi.

Wakati huo huo, kocha Pep Guardiola wa Manchester City ameeleza kufurahishwa kwake na kiwango cha winga wake, Riyad Mahrez ambaye timu yake ya Algeria imetinga hatua ya nusu-fainali ya AFCON.

Guardiola anayejiandaa kuwakaribisha wachezaji wake kwa maandalizi ya msimu mpya alisema kiwango cha Mahrez kimeimarika zaidi nchini hapa, huku akimtarajia kukiendeleza zaidi atakaporudi klabuni.

Ushindani

Klabuni, Mahrez anashindania namba dhidi ya Leroy Sane, Raheem Sterling na Bernardo Silva.

Mahrez aliyefunga bao nzuri na kuisaidia Algeria kuibuka na ushindi wa 3-0 dhidi ya Guinea, Jumapili na kufuzu kwa robo-fainali, juzi Alhamisi usiku alikuwa katika kikosi cha timu hiyo kilichoibuka na ushindi wa 4-3 dhidi ya Ivory Coast na kutinga hatua ya nusu-fainali.

Lakini iwapo Algeria itaipiga Nigeria na kufuzu kwa fainali ya michuano hiyo, basi inamaanisha Mahrez hataweza kujiunga na Manchester City mapema, ikizingatiwa kwamba lazima nyota huyo apewe lilikizo ya wiki tatu kabla ya kurudi katika klabu hiyo ya ligi kuu ya Uingereza (EPL).

Hali hiyo itawaweka mabingwa hao katika wakati ngumu ikikumbukwa kwamba vijana hao wa Guardiola wamepangiwa kukutana na Liverpool katika mchezo wa Community Shield Agosti 4 kabla ya ligi kuanza rasmi siku sita baadaye, ambapo wamepangiwa kukutana na West Ham United ugenini.