Michezo

Nimelazimishwa kubaki Barcelona – Messi

September 7th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na MASHIRIKA

NYOTA Lionel Messi, 33, atasalia ugani Camp Nou kuvalia jezi za Barcelona msimu ujao wa 2020-21.

Hata hivyo, huenda muhula huo ukawa wa mwisho kwa mfumaji na nahodha huyo kusakatia soka miamba hao wa Ligi Kuu ya Uhispania (La Liga) baada ya kufichua kwamba hahusiani vyema na rais wa kikosi hicho, Josep Maria Bartomeu.

Kwa mujibu wa gazeti la Mundo Deportivo nchini Uhispania, Messi atakuwa radhi kuanzisha mazungumzo na vikosi vingine kuanzia Januari 2021 kuhusu uwezekano wa kumsajili mwishoni mwa Julai 2021 iwapo Bartomeu hatajiuzulu.

Ingawa hivyo, gazeti la Marca limeshikilia kwamba Jorge, ambaye ni baba na wakala wa Messi, amepania kuzungumza na Barcelona kwa siku kadhaa zijazo katika juhudi za kutafuta mwafaka utakaomshuhudia mwanawe akistaafu soka akiwa mchezaji wa mabingwa hao mara 26 wa La Liga.

Mnamo Agosti 25, Bartomeu alikiri kwamba angeng’atuka mamlakani iwapo Messi angejitokeza hadharani na kuungama kuwa ndiye kiini cha kusuasua kwa Barcelona ambao tayari wameagana na wanasoka matata Arthur Melo (Juventus), Luis Suarez (Juventus) na Ivan Rakitic (Sevilla).

“Ni muda mrefu tangu mradi wowote wa kuhakikisha ustawi wa klabu uanzishwe na kufanikishwa na Barcelona chini ya Bartomeu. Kikosi kimekuwa ngome ya mizozo kati ya wasimamizi, vinara wa benchi ya kiufundi na wachezaji,” akasema Messi.

Tangazo la Messi kutaka kuhama Barcelona lilivutia klabu za Juventus, PSG, Inter Milan na Manchester City waliokuwa radhi kumpa ujira wa Sh196 milioni kwa wiki na Sh10 bilioni kwa mwaka.

Nyota huyo alipania kutumia kifungu kwenye mkataba wake kinachomruhusu kuagana na Barcelona bila ada yoyote. Hata hivyo, Barcelona wameshikilia kuwa supastaa huyo angali na mwaka mmoja zaidi kwenye mkataba wake kwa kuwa aliwaarifu kuhusu mpango wake wa kuondoka baada ya tarehe ya makataa (Juni 10).

Aidha, vinara wa Ligi Kuu ya Uhispania (La Liga) walisema kipengele kinachohitaji kikosi chochote kuweka mezani kima cha Sh89 bilioni ili kumtwaa Messi bado kinafanya kazi na lazima kizingatiwe katika mipango yote ya kurasimisha uhamisho wake.

“Nitaendelea kuwa mchezaji wa Barcelona kwa sababu haiwezekani kwa kikosi chochote kutoa Sh89 bilioni kwa minajili ya huduma zangu,” akatanguliza.

“Njia nyingine ya kuondoka Camp Nou ni Kwenda kutafuta haki mahakamani. Lakini nisingetaka kufuata mkondo huo kwa sababu naistahi sana Barcelona. Kikosi kilichonipa malezi ya soka na kila kitu,” akasema.

“Isitoshe, mipango ya kuhama iliathiri sana familia yangu. Mke na watoto wamekuwa wakilia sana tangu niweke bayana maazimio ya kuondoka Barcelona,” akaongeza Messi.

Licha ya kutofurahia maisha ya sasa mjini Catalonia, Messi ameapa kujitahidi kadri ya uwezo wake kutambisha Barcelona msimu ujao chini ya mkufunzi mpya Ronald Koeman aliyemrithi Quique Setien aliyetimuliwa baada ya masogora wake kudhalilishwa 8-2 na Bayern Munich kwenye robo-fainali za Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) msimu huu wa 2019-20.

Matokeo duni ya Barcelona msimu huu yalishuhudia kikosi hicho kikikosa kutia kapuni taji lolote kwa mara ya kwanza tangu 2008. Hii ni baada ya kuambulia nafasi ya pili kwenye Ligi Kuu ya Uhispania (La Liga) na kubanduliwa mapema na Athletic Bilbao kwenye kivumbi cha Copa del Rey.

Messi, ambaye ni mshindi mara sita wa taji la Ballon d’Or ambalo mchezaji bora zaidi duniani hupokezwa, aliwajibishwa na Barcelona kwa mara ya kwanza mnamo 2004 na amewaongoza kunyanyua ubingwa wa UEFA mara nne.

Alijiunga na Barcelona akiwa na umri wa miaka 13 pekee na amefungia waajiri wake jumla ya mabao 634 kutokana na mechi 730 zilizopita na ndiye mwanasoka anayejivunia historia ya mafanikio makubwa zaidi ugani Camp Nou baada ya kuwanyanyulia kikosi hicho jumla ya mataji 33.