Michezo

Nisingekuwa sogora bila Messi – Ronaldo

August 23rd, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na MASHIRIKA

LIBSON, Ureno

GUNGE Cristiano Ronaldo alikiri Jumatano kuwa uhasama wa muda mrefu na Lionel Messi umemfanya kuwa “mchezaji bora” na kuwa anafurahia kuwa na uhusiano “mzuri” na shujaa huyo wa Argentina.

Hata hivyo, nyota huyo wa Ureno, ambaye mchango wake Real Madrid haukutofautiana na ule wa Messi katika klabu ya Barcelona kabla ahamie Juventus, alikiri kuwa hajawahi kujishughulisha kuwa rafiki ya Messi.

“Kwa kweli, napendezwa na mafanikio amepata katika uchezaji wa kabumbu na kwa maoni yake, tayari alizungumzia kusikitishwa kwake nilipoondoka nchini Uhispania kwa sababu aliukubali uhasama wetu,” Ronaldo aliambia runinga ya TVI nchini Ureno.

“Ni uadui mzuri, lakini ni kitu cha kawaida – Michael Jordan alikuwa na uhasama katika mpira wa vikapu, pia haikuwa tofauti kati ya madereva wa magari ya langalanga Ayrton Senna na Alain Prost. Kile kiliwaleta pamoja ni kuwa wote walikuwa na uadui mzuri.”

Ronaldo na Messi wameshinda tuzo ya kifahari ya mwanasoka bora duniani ya Ballon d’Or mara tano kila mmoja, kitu ambacho kinawasaidia kila mmoja wao kunawiri.

“Sina taswishi kuwa Messi amenifanya kuwa mchezaji bora na pia najua amenufaika vivyo hivyo kutoka kwangu. Ninaposhinda mataji, lazima iwe inamuuma sana na pia mimi huhisi hivyo anaposhinda,” alisema.

“Niko na uhusiano mzuri wa kisoka naye kwa sababu tumekuwa tukipata ufanisi huu katika kipindi cha miaka 15.

Aliongeza, “Hatujawahi kula chakula pamoja, lakini sioni kwanini hatuwezi kufanya hivyo siku za usoni. Sioni tatizo na hilo.”

Aidha, Messi huenda akarejea kutandazia Barca soka dhidi ya Real Betis siku ya Jumapili baada ya kupona jeraha la mguu.

Mchezaji huyu mbunifu amekuwa mkekani tangu Agosti 5 na alikosa mchuano wa kufungua msimu timu yake ikipoteza 1-0 dhidi ya Athletic Bilbao.

Messi ajiunga na wenzake kufanya mazoezi

Hata hivyo, Messi aliungana na wachezaji wenzake kwa mazoezi makali Jumatano kujiandaa kwa mechi dhidi ya Betis.

“Tumekuwa tukisubiri habari hizi na hatimaye zimefika kwa sababu Messi alirejelea mazoezi na wenzake uwanjani Ciutat Esportiva Joan Gamper,” taarifa katika tovuti ya Barcelona.

“Ilikuwa mara ya kwanza amefaulu kufanya mazoezi makali tangu ajeruhi mguu wake wa kulia mnamo Agosti 5. Alikuwa kivutio katika uwanja huo wa mazoezi ambako pia kikosi cha kwanza kilikaribisha wachezaji Inaki Pena, Chumi, Carles Perez na Abel Ruiz kutoka timu ya pili ya Barcelona (Barcelona B) pamoja na chipukizi matata Ansu Fati kutoka timu ya wachezaji wasiozidi umri wa miaka 19.

“Timu hii itakuwa na mapumziko Alhamisi na kurejelea mazoezi Ijumaa asubuhi, huku tukiandaa kipindi kimoja cha mazoezi Jumamosi kabla ya kukabiliana na Real Betis katika mechi ya kwanza nyumbani uwanjani Camp Nou mnamo Jumapili.”