NTV kuwapa raha mashabiki kwa kuonyesha mechi za Kombe la Dunia
Na JOHN ASHIHUNDU
Sasa ni nafuu kwa mashabiki sugu wa soka nchini baada ya runinga ya NTV kutangaza kwamba itapeperusha moja kwa moja mechi za Kombe la Dunia zitakazofanyika nchini Urusi kuanzia Juni 14.
Alhamisi, Shirika la Habari na Utangazaji la Nation Media Group (NMG) lilitia saini makubaliano na kituo cha kupeperusha habari za spoti cha Kwese Free Sports ili kuonyesha moja kwa moja mechi za fainali hizo.
Mechi hizo ni pamoja na zile za makundi zitakazohusisha timu zitakazowakilisha bara Afrika, za nusu-fainali na fainali. Mechi hizo zitachezewa katika miji tofauti ikiwemo jiji kuu la Moscow, Kransnodar, Kazan, Saint Petersburg, Sochi na Yaroslavi.
“Hii imewezekana baada ya mkataba baina ya mashirika haya maarufu ya habari. Nina hakika baada ya kumalizika kwa fainali hizo tutafurahia faida kutoka kwa mashabiki,” Meneja Mkuu wa Kwese Sports, Monica Ndung’u, alieleza.
“Ni fursa kubwa kwa watazamaji wetu kushuhudia mechi hizi kubwa duniani wakistarehe katika sehemu mbalimbali, hata wakiwa manyumbani mwao,” alisema Afisa Mkuu wa NMG, Stephen Gitagama.
“NTV imejitolea kuwafurahisha wafuasi wake kwa kuonyesha mechi hizo ambazo pia zitawasaidia wale wasio na uwezo wa kifedha kuzitazama bila malipo.
Kwa upande wangu, nitazifuatilia kwa makini ili nijiongezee ujuzi zaidi wakati huu ninapojiandaa kurejea katika timu ya taifa,” alisema Musa Mohammed aliyekuwa nahodha wa kikosi cha Harambee Stars kilichotwaa taji la Cecafa Senior Challenge Cup, mwaka uliopita.
Timu 32 zitashiriki katika fainali hizo, zikiwemo tano kutoka Afrika ambazo ni Nigeria, Senegal, Misri, Morocco na Tunisia.
Mabingwa watetezi Ujerumani, pamoja na Brazil, Ureno, Ublegiji, Ufaransa, Argentina na Uingereza zinawekewa nafasi kubwa.
Mashabiki watapata fursa ya kuwashuhudia nyota kadhaa wakiwemo Cristiano Ronaldo, Lionel Messi, Mo Salah, Saidio Mane, Harry Kane na Eden Hazard ambao watakuwa wakichezea timu za mataifa yao.
Makundi: Kundi A: Urusi, Misri, Saudia; Kundi D: Argentina, Croatia, Iceland, Nigeria; Kundi G: Ubelgiji, Uingereza, Tunisia, Panama; Kundi H: Poland, Colombia, Senegal na Japan.