Michezo

NUSU-FAINALI FA: Manchester United kuvaana na Chelsea huku Arsenal ikionana na mabingwa watetezi Manchester City

June 29th, 2020 Kusoma ni dakika: 1

Na CHRIS ADUNGO

MANCHESTER United watakutana na Chelsea, nao Arsenal wavaane na mabingwa watetezi Manchester City katika nusu-fainali za Kombe la FA msimu huu.

Droo hiyo iliyofanywa Jumapili ya Juni 28, 2020 inajumuisha vikosi vitatu kati ya vinne vinavyojivunia mafanikio makubwa zaidi katika historia ya kipute hicho.

Arsenal wanashikilia rekodi ya kujizolea ufalme wa Kombe la FA kwa mara nyingi zaidi (misimu 13).

Man-United waliojikatia tiketi ya nusu-fainali kwa kuwabandua Norwich City wanajivunia ubingwa wa Kombe la FA mara 12 huku Chelsea waliozidi maarifa Leicester City kwenye robo-fainali wakiwa washindi mara nane.

Mechi zote mbili za nusu-fainali zimepangiwa kutandazwa uwanjani Wembley kati ya Julai 18-19, 2020. Fainali imepangiwa kusakatwa mnamo Jumamosi ya Agosti 1, 2020 katika uwanja uo huo wa Wembley, Uingereza.

Droo ya nusu-fainali za Kombe la FA ilifanywa wakati wa mapumziko ya mechi kati ya Newcastle United na Man-City ambayo ilishuhudia masogora wa kocha Pep Guardiola wakisajili ushindi wa mabao 2-0 yaliyofumwa wavuni na kiungo Kevin de Bruyne na mshambuliaji Raheem Sterling.

Mechi hiyo kati ya Newcastle na Man-City ilichezewa uwanjani St James’ Park baada ya Arsenal kuwapepeta Sheffield United 2-1 ugani Bramall Lane nao Chelsea kuzamisha chombo cha Leicester uwanjani King Power.

Mabao ya Arsenal yalimiminwa kimiani kupitia kwa fowadi Nicolas Pepe aliyefunga kupitia penalti ya kipindi cha kwanza kabla ya Dani Ceballos kucheka na nyavu mwishoni mwa kipindi cha pili.

Nusu-fainali kati ya Man-United na Chelsea ni marudio ya fainali ya Kombe la FA mnamo 2018 iliyoshuhudia Chelsea wakiibuka washindi.

DROO YA NUSU-FAINALI YA KOMBE LA FA:

Man-United na Chelsea

Arsenal na Man-City