Nyota waliovuma 2018/19 kutiwa katika mizani Ijumaa
Na CHRIS ADUNGO
ORODHA ya wawaniaji watatu wa kila kitengo katika tuzo za Wachezaji Bora wa Ligi Kuu ya Kenya (KPL) 2019 inatarajiwa kutolewa Ijumaa.
Hafla ya kuzawidiwa kwa masogora hao waliotia fora zaidi katika kampeni za msimu uliopita imeratibiwa kufanyika Jumatatu ya wiki ijayo.
Katika orodha ya awali kabisa ya wawaniaji watano wa kila kitengo, Bandari walijivunia wachezaji wengi zaidi hasa ikizingatiwa ukubwa wa mafanikio yao msimu jana.
Chini ya mkufunzi Bernard Mwalala, kikosi hicho cha Pwani ya Kenya kilitia kapuni ufalme wa Shield Cup na pia kukamilisha kampeni za KPL katika nafasi ya pili nyuma ya Gor Mahia waliotawazwa mabingwa kwa mara ya 18.
Ufanisi wa Bandari katika kivumbi cha Shield Cup uliwakatia tiketi ya kuwakilisha Kenya katika kampeni za Kombe la Mashirikisho barani Afrika (CAF Confederations Cup) mwaka 2019.
Bandari kwa sasa wanajiandaa kwa marudiano na Ahli Shendi ugenini baada ya kuambulia sare tasa na miamba hao wa Sudan katika mrechi ya kwanza jijini Nairobi wikendi iliyopita.
Orodha ya wawaniaji wa tuzo za KPL 2019 pia inawajumuisha baadhi ya wachezaji waliosajiliwa na vikosi mbalimbali nje ya Kenya muhula huu baada ya kutambisha vikosi vyao vya KPL msimu jana.
Farouk Shikhalo wa SC Yanga nchini Tanzania anatazamiwa kuhifadhi taji la Kipa Bora wa Mwaka.
KIPA BORA: Faruk Shikalo (awali Bandari), Justin Ndikumana (awali Sofapaka), Kevin Omondi (awali Sony Sugar), Samuel Odhiambo (Western Stima), Morgan Alube (Chemelil Sugar), na Omar Adisa (KCB).
BEKI BORA: Brian Otieno (Bandari), David Owino (Mathare), Faina Jacobs (Sofapaka), Kelvin Wesonga (Sony Sugar), Joash Onyango (Gor), Harun Shakava (awali Gor).
VIUNGO BORA: Francis Kahata (awali Gor), Cliff Nyakea (awali Mathare), Bonface Muchiri (Tusker), Danson Chatambe (awali Zoo Kericho), Whyvone Isuza (AFC Leopards), na Abdallah Hassan (Bandari).
CHIPUKIZI: David Majak (Tusker), Jackson Dwang (Nzoia) Moses Mudavadi (Bandari), Daniel Sakari (awali KK Homeboyz), na Joshua Nyatini (awali SoNy).
MCHEZAJI BORA ZAIDI: Francis Kahata (awali Gor), Joash Onyango (Gor), Umaru Kasumba (awali Sofapaka), Enosh Ochieng (Ulinzi), Allan Wanga (KK Homeboyz) na Boniface Muchiri (Tusker).
KOCHA BORA: Hassan Oktay (awali Gor), John Baraza (Sofapaka), Patrick Odhiambo (awali SoNy), Benard Mwalala (Bandari), Robert Matano (Tusker), Francis Kimanzi (awali Mathare).