OLE NDIYE! Ni rasmi sasa mikoba ya United ni ya Gunnar
Na MASHIRIKA
MANCHESTER, Uingereza
Baada ya kuhudumu kama kocha mshikilizi wa Manchester United kwa muda wa miezi minne, Ole Gunnar Solskjaer sasa ameteuliwa rasmi kuwa kocha wa kudumu wa klabu hiyo.
Mara tu baada ya kupewa mkataba wa miaka mitatu, mashabiki wa klabu hiyo walijitokeza mitandaoni kumtakia kocha huyo heri njema katika kazi yake.
Miongoni mwa jumbe hizo ni kutoka kwa Paige Williams aliyesema: “Ole kwenye usukani. Ni uamuzi bora wa Manchester United!”
“Ni habari tulizongojea kwa hamu!! Twende Ole!#GGMU,” alisema Ali Hameed.
“Bila shaka atafanya kazi nzuri, ni mtu anayependa hii timu, baada ya kuichezea kabla ya kuwa kocha. Pongezi, Ole Gunnar Solskjaer!” aliongeza Joyce Crawford.
Okeke Samuel: “Karibu mkubwa! Sasa wacha kazi ianze.”
Dava Southward: “Hongera, Ole. Kushindwa mara moja ligini tangu Desemba. Endelea tu kuokota pointi!”
Tony Wood: “Habari njema zaidi za mwaka.”
Victor Omwambi: “Nilijua ni yeye atapewa. Ni mmoja wetu, anafahamu vyema kaida na desturi za klabu yetu. Bwana Ole, tufanikishie hili.”
Glyn John: “Hongera, Ole, unastahili jukumu hili….. sasa unaweza kuanza kujipanga kwa msimu ujao na zaidi. Kila la heri, ebu turudishie taji letu…”
Baada ya kupewa jukumu hili, kuna wachezaji kadhaa ambao huenda wakalazimika kuanza kutafuta klabu za kuchezea.
Miongoni mwao ni Alexis Sanchez ambaye kiwango chake kimeshuka kwa kiasi kikubwa. Raia huyo wa Chile amekuwa haingiani na wenzake tangu atue Old Trafford Januari 2018.
Amefunga mabao mawili pekee baada ya kupewa nafasi katika mechi 23, msimu huu, licha ya pesaa nyingi anazolipwa.
Pia kuna Fred ambaye ni majuzi tu alipoonyesha kiwango kizuri katika ushindi wao wa 3-1 dhidi ya PSG tangu anunuliwe kutoka Shakhtar Donetsk msimu uliopita.
Alipata nafasi kucheza mechi hiyo kutokana na majeraha kwa nyota kadhaa waliokuwa nje. Mchezaji mwingine ni Juan Mata ambaye mkataba wake unamalizika mwishoni mwa msimu huu.
Wakati uo huo, nyota wa Manchester United, Ander Herrera amekiri kuwa mwenendo wao wa kushangaza katika michuano ya Klabu Bingwa Ulaya msimu huu unachangiwa pakubwa na historia ya klabu ya Chelsea.
United walifanya maajabu kwa kuing’oa PSG katika hatua ya 16 Bora ambapo iligeuza matokeo ya kufungwa 2-0 nyumbani kabla ya kushinda 3-1 ugenini.
Baada ya ushindi huo wa kihistoria, vijana hao wa kocha Ole Gunna Solskjaer wamepangiwa kucheza na FC Barcelona katika hatua ya robo-fainali, lakini bado ina imani ya kuwatoa jasho mibabe hao wa Uhispania.
Herrera alisema kuwa, United wanatumia historia ya Chelsea ilipotwaa Ligi ya Klabu Bingwa mnamo 2012 na kuwashangaza wale ambao walikuwa hawaiamini timu hiyo ilipokuwa chini ya Robero Di Matteo.
“Kwenye Ligi Kuu ya Uingereza hatuna uwezo wa kutwaa taji, lakini bado tuna imani ya kushinda taji la Ligi ya Mabingwa,” alisema Herrera.
“Tunakumbuka jinsi Chelsea ya Di Matteo ilivyokosa wa kuiamini lakini ikasonga mbele na kutwaa ubingwa wa 2012,” aliongeza.