Oliech akosa nafasi kwa kikosi cha AFCON na CHAN
Na GEOFFREY ANENE
HAKUNA nafasi kwa mfungaji bora wa Kenya Dennis Oliech katika timu ya Kocha Sebastien Migne, ambaye ametangaza kikosi cha wachezaji 25 wanaosakata humu nchini kwa majukumu kimataifa ya AFCON 2019 na CHAN 2020.
Kenya itaalikwa na Ghana katika mechi yake ya mwisho ya kufuzu Kombe la Bara Afrika (AFCON) 2019 ya Kundi F mjini Kumasi mnamo Machi 22.
Vijana wa Migne watapepetana na Burundi nyumbani na ugenini katika mechi za kuwania tiketi ya kushiriki Kombe la Bara Afrika kwa wachezaji wanaocheza katika mataifa ya (CHAN) 2020. Shirikisho la Soka barani Afrika (CAF) linatatarajiwa kutangaza tarehe za mechi ya Stars dhidi ya Burundi hivi karibuni.
Wachezaji 17 kati ya 25 walioitwa na Mfaransa Migne watashiriki kipindi cha kwanza cha mazoezi kesho katika Taasisi ya Mafunzo ya Kifedha (KSMS) mtaani Ruaraka.
Francis Kahata, Philemon Otieno na Joash Onyango hawatahudhuria kipindi cha Jumanne kwa sababu klabu yao ya Gor Mahia imeratibiwa kualika Western Stima katika mechi ya Ligi Kuu mnamo Februari 20.
Elvis Nandwa (Ulinzi Stars), Abdallah Hassan (Bandari), Farouk Shikalo (Bandari), Allan Wanga (Kakamega Homeboyz) na Bernard Ochieng (Vihiga United), ambao klabu zao zinapatikana nje ya Nairobi, pia hawatahudhuria kipindi cha kwanza cha mazoezi. Watajiunga na timu juma lijalo.
Oliech, 34, ambaye amefungia Kenya mabao 34, alistaafu kutoka soka Machi 24 mwaka 2016 kabla ya kubatilisha uamuzi huo na kujiunga na Gor kwa kandarasi ya miaka miwili hapo Januari 2, 2019. Amefungia Gor mabao mawili ligini na moja dhidi ya miamba wa Misri Zamalek katika Klabu Bingwa Afrika.
Baada ya Oliech kuonyesha mashabiki wa Kenya bado hajakuwa butu, wengi walianza kupigia debe wakisema anastahili kujumuishwa na Migne katika timu ya taifa tena hasa kwa kipute cha AFCON.
Kikosi: Makipa – Brian Bwire (Kariobangi Sharks), John Oyemba (Kariobangi Sharks), Farouk Shikalo (Bandari); Mabeki – Andrew Juma (Mathare United), David Owino (Mathare United), Philemon Otieno (Gor Mahia), Joash Onyango (Gor Mahia), Elvis Nandwa (Ulinzi Stars), Michael Kibwage (KCB), Benard Ochieng (Vihiga United); Viungo – Francis Kahata (Gor Mahia), James Mazembe (Kariobangi Sharks), Duke Abuya (Kariobangi Sharks), Roy Okal (Mathare United), Cliff Nyakeya (Mathare United), John Avire (Sofapaka), Dennis Odhiambo (Sofapaka), Teddy Osok (Wazito), Whyonne Isuza (AFC Leopards), Jafari Owiti (AFC Leopards), Abdallah Hassan (Bandari); Washambuliaji – Sydney Lokale (Kariobangi Sharks), Piston Mutamba (Sofapaka), Allan Wanga (Kakamega HomeBoyz), David Juma (Tusker).