• Nairobi
  • Last Updated May 20th, 2024 9:16 PM
Oliech hawezi kuteuliwa kuwa naibu kocha – Gor Mahia

Oliech hawezi kuteuliwa kuwa naibu kocha – Gor Mahia

NA CECIL ODONGO

UONGOZI wa Gor Mahia umekanusha kwamba mshambulizi mkongwe Dennis Oliech amepokezwa kazi ya naibu mkufunzi huku hatima ya kocha Hassan Oktay ikiwa haijulikani.

Afisa Mkuu Mtendaji wa K’Ogalo Omondi Aduda na Mwekahazina Sally Bollo wamekemea habari hizo wakisema Oliech amepona jeraha na amerejea mazoezini kama mchezaji wala si naibu kocha.

“Oliech atakuwa naibu kocha kivipi ilhali hana cheti chochote cha ukufunzi. Nimetoka mazoezini leo asubuhi (jana) na Oliech anafanya mazoezi kama wachezaji wengine. Tunasubiri siku chache alizoomba Oktay kutatua masuala ya kibinafsi ya nyumbani ziishe ili tufahamu iwapo atarudi au la. Kwa sasa yeye bado ni kocha na hilo litabadilika tu iwapo atatueleza vinginevyo jinsi tulivyokubaliana naye,” akasema Bollo.

Odhiambo

Kauli yake iliungwa mkono na Aduda ambaye alisema kaimu kocha Patrick Odhiambo atachukua usimamizi wa timu hadi Oktay arejee na Oliech hajapewa wadhifa wowote kwenye usimamizi wa timu.

“Nimeona baadhi ya mitandao inasema meneja wa timu ndiye alimteua Oliech kusaidia katika ukufunzi na habari hizo ni uongo. Tangu lini meneja wa timu akawa na jukumu la kumteua naibu kocha? Oliech amekuwa mazoezini na hana vyeti vya ukufunzi kumwezesha kuwa kocha,” akasema Aduda.

Maafisa hao pia walikanusha tetesi kwamba Oktay hakufurahia sajili wapya timu, baadhi ya wachezaji wakidaiwa kupewa mikataba bila idhini ya Mturuki huyo.

Wakati huo huo baadhi ya mashabiki kwenye ukumbi wa klabu hiyo wamekerwa na madai kwamba Oliech amepewa kazi ya naibu mkufunzi, wakishikilia kwamba uongozi wa klabu ndio umechangia Oktay kutoroka.

Akizungumza na Taifa Leo Jumanne, Oktay alipuuza tetesi kwamba ameitoroka Gor Mahia ila akasisitiza kwamba atazungumza na Mwenyekiti Ambrose Rachier iwapo masuala anayoyashughulikia hayatakamilika kwa muda aliokusudia.

You can share this post!

Kocha alalama kutohusishwa na usajili Spurs

Kashiwa Reysol ya Olunga sasa yaongoza vita vya kurejea...

adminleo