• Nairobi
  • Last Updated May 9th, 2024 5:17 PM
Olunga achezeshwa dakika 10 za mwisho Kashiwa ikigawana alama moja dhidi ya Oita Trinita

Olunga achezeshwa dakika 10 za mwisho Kashiwa ikigawana alama moja dhidi ya Oita Trinita

Na GEOFFREY ANENE

NYOTA Michael Olunga alichezeshwa dakika 10 pekee timu yake ya Kashiwa Reysol ikikamilisha mechi tano za nyumbani bila ushindi baada ya kutoka 1-1 dhidi ya Oita Trinita kwenye Ligi Kuu ya Japan (J1 League) uwanjani Sankyo Frontier, Jumatano.

Olunga, ambaye anaongoza jedwali la wafungaji wa mabao kwenye ligi hiyo ya klabu 18, aliingizwa uwanjani kama mchezaji wa akiba katika nafasi ya Hiroto Goya. Mshambuliaji huyo Mkenya huyo anayefahamika kwa jina la utani kama Engineer, alikuwa amesakata mechi nzima mara nne mfululizo kabla ya kupunguziwa dakika uwanjani. Amekamilisha dakika 180 bila bao baada ya kuwa katika kikosi kilicholimwa 1-0 na Nagoya Grampus mnamo Desemba 9.

Huku mechi kali zaidi ya Oita dhidi ya Cerezo Osaka (Desemba 12), Sanfrecce Hiroshima (Desemba 16) na mabingwa Kawasaki Frontale (Desemba 19) zikinukia, kocha Mbrazil Nelson Baptista aliamua kuwaweka kitini wachezaji muhimu Olunga na kiungo mbunifu Ataru Esaka. Wachezaji wengi walioanza kwenye benchi dhidi ya Nagoya walipata fursa ya kuanza dhidi ya Oita.

Olunga alipata nafasi yake dakika ya 85, sekunde chache baada ya wageni Oita kusawazisha bao lililokuwa limefungwa na Goya dakika ya 47.

Mbali na kutaja Olunga na Esaka kwenye benchi, Nelsinho pia alibadilisha mfumo wake wa kawaida wa 4-2-3-1 na kutumia 3-4-2-1 huku Goya akitumiwa katika nafasi ya Olunga. Oita pia ilitumia mfumo wa Kashiwa. Timu hizi zilicheza kwa tahadhari kipindi cha kwanza kilichotamatika 0-0.

Goya aliweka Kashiwa kifua mbele dakika mbili baada ya kipindi cha pili kuanza akifuma wavuni kichwa kisafi.

Hayato Nakama alipoteza nafasi ya wazi ya kuimarisha uongozi wa Kashiwa sekunde chache baadaye kabla ya Oita kufanya mabadiliko yote matano kati ya dakika ya 62 na 76 ikipumzisha Ryosuke Tone, Kaoru Takayama, Ryosuke Maeda, Kazushi Mitsuhira na kuingiza Yuto Misao, Tatsuya Tanaka, Kobayashi na Yamato Machida katika nafasi zao.

Kashiwa ilifanya badiliko lake la kwanza dakika ya 81 pale ilipomuingiza Kamiya katika nafasi ya Nakama sekunde chache baada ya Oita kusawazisha 1-1 kupitia kwa shuti la Tomoki Iwata. Olunga aliingia uwanjani zikisalia dakika tano muda wa kawaida ukatike akichukua nafasi ya Goya. Alipata nafasi nzuri sekunde chache baadaye baada ya kupokea pasi kutoka kwa Mbrazil Cristiano, lakini Oita iliondosha hatari hiyo kwa haraka.

Baada ya kipenga cha mwisho kulia dakika ya tano ya ziada ilipokatika, Olunga alisalia bado mabao tisa mbele ya Mbrazil Everaldo katika vita vya kuibuka mfungaji bora. Everaldo anachezea Kashima Antlers.

Kashiwa imepaa nafasi moja hadi nambari saba kwenye jedwali kwa alama 48 na kusukuma Hiroshima katika nafasi ya nane kwa tofauti ya ubora wa magoli. Oita inasalia katika nafasi ya 11 kwa alama 38.

You can share this post!

Timu ‘B’ ya Chelsea yapiga Krasnodar na kusonga...

Polisi ashtakiwa kwa kumjeruhi mwenzake