• Nairobi
  • Last Updated April 27th, 2024 4:54 PM
Olunga aongoza Kashiwa kupiga Kashima Antlers akifikisha mabao 25 Ligi Kuu ya Japan

Olunga aongoza Kashiwa kupiga Kashima Antlers akifikisha mabao 25 Ligi Kuu ya Japan

Na GEOFFREY ANENE

MSHAMBULIAJI matata wa Kenya, Michael Olunga anazidi kutesa makipa kwenye Ligi Kuu ya Japan baada ya kupachika bao lake la 25 ligini na 26 kwa jumla msimu huu Kashiwa Reysol ikibwaga wenyeji Kashima Antlers 4-1 Jumatano.

Vijana wa kocha Nelsinho Baptista, ambao hawakuwa na ushindi dhidi ya Kashima katika mechi tano zilizopita, walitawala ugenini kupitia kwa mabao ya Kengo Kitazume, Olunga, Cristiano na nguvu-mpya Yuta Kamiya.

Reysol, ambayo ilikuwa imepoteza michuano mitatu mfululizo dhidi ya wapinzani hao kwa jumla ya mabao 12-6, ilituma onyo mapema ilipobisha lango la Kashima mara 10 dhidi ya mashambulizi manne kutoka kwa wenyeji wao kabla ya kupata bao la kwanza kupitia kwa Kengo Kitazume dakika ya 26.

Olunga, ambaye anaongoza ufungaji wa mabao kwenye ligi hiyo maarufu kama J1 League, pamoja na kiungo mbunifu Ataru Esaka na Yusuke Segawa, ambaye alikuwa akirejea katika kikosi cha kuanza baada ya mechi moja, walipata nafasi kadha nzuri kabla ya bao la Kitazume kupeleka Kashiwa bao 1-0 juu wakati wa mapumziko.

Kashiwa haikulegeza kamba katika kipindi cha pili, ingawa ilipata pigo wakati Juan Alano alisawazisha baada ya kipa kutoka Korea Kusini Seung-Gyu Kim kutema mpira dakika ya 56.

Olunga, 26, ambaye aliibuka mchezaji bora wa ligi hiyo wa mwezi Agosti, alirejesha Kashiwa kifua mbele 2-1 dakika ya 75. Alipokea pasi kutoka kwa Esaka na kuikamilisha kwa ustadi.

Kashima ilipoteza nafasi ya wazi dakika chache baadaye kabla ya Mbrazil Cristiano kuongeza bao la tatu dakika ya 82 pia kutokana na pasi ya Esaka baada ya shambulio la Kashima kuzimwa. Olunga, Esaka na Cristiano walishirikiana vyema katika idara ya mbele na kuhangaisha Kashima.

Kitumbua cha Kashima kiliingia mchanga pale Kamiya, ambaye alijaza nafasi ya Esaka dakika ya 85, alipoongeza bao la nne dakika ya kwanza ya majeruhi.

Baada ya mechi hiyo iliyosakatwa mbele ya mashabiki 4, 327 uwanjani Kashima Soccer Stadium, Kashima ilitupwa chini nafasi moja hadi nambari tano kwa alama 52. Mabingwa Kawasaki Frontale walikung’uta nambari mbili Gamba Osaka 5-0 katika mechi ya timu mbili za kwanza. Kawasaki imevuna alama 75, pointi 17 mbele ya Gamba nayo Nagoya Grampus ni ya tatu kwa alama 53. Cerezo Osaka ni ya nne baada ya kulemea Oita Trinita 1-0.

Kashiwa imesalia katika nafasi ya 10 kwa alama 44 kutokana na mechi 28. Vijana wa Nelsinho watazuru wavuta-mkia Vegalta Sendai katika mechi ijayo mnamo Desemba 1. Mechi hiyo ilikuwa imepangwa kuchezwa Novemba 3, lakini ikaahirishwa baada ya kambi ya Kashiwa kuripoti visa 16 vya maambukizi ya virusi vya corona.

Vikosi:

Kashiwa Reysol

Kim Seung Gyu; Kengo Kitazume, Takuma Ominami, Tatsuya Yamashita, Taiyo Koga; Richardson, Masatoshi Mihara, Cristiano, Yusuke Segawa; Ataru Esaka, Olunga.

Wachezaji wa Akiba – Golikipa Haruhiko Takimoto, mabeki – Jiro Kamata, Shunki Takahashi, Naoki Kawaguchi, viungo – Yuta Kamiya, Hayato Nakama, fowadi Hiroto Goya.

Kashima Antlers

Yuya Oki; Kei Koizumi, Tomoya Inukai, Tatsuki Nara, Shuto Yamamoto; Kento Misao, Leo Silva, Juan Alano, Shoma Doi; Everaldo, Ueda. Wachezaji wa Akiba – Golikipa Kwoun Sun-tae; mabeki – Rikuto Hirose, viungo – Ryota Nagaki, Yasushi Endo, Yuta Matsumura, Shintaro Nago; fowadi – Sho Ito.

You can share this post!

Shujaa waalikwa kucheza Uhispania na Ufaransa kabla ya...

Rais amfokea Kinoti vikali