Olunga arejea kuanza mechi Kashiwa Reysol ikiumiza nyasi bure dhidi ya Cerezo
Na GEOFFREY ANENE
NYOTA Michael Olunga alirejea katika kikosi cha wachezaji 11 wa kwanza timu ya Kashiwa Reysol ikigawana alama katika sare ya 0-0 dhidi ya wenyeji Cerezo Osaka kwenye Ligi Kuu ya Japan, Jumamosi.
Mshambuliaji huyo Mkenya pamoja na kiungo mbunifu Ataru Esaka walitiwa kwenye benchi katika mechi dhidi ya Oita Trinita mnamo Desemba ambayo ilitamatika 1-1. Olunga, ambaye sasa hajaona lango katika michuano mitatu mfululizo, aliingizwa katika dakika ya 84 dhidi ya Oita, huku Esaka akikosa kutumiwa kabisa.
Kocha Nelson Baptista alirejesha wawili hao kwenye kikosi cha kuanza mechi Jumamosi akimchezesha Olunga dakika zote 90. Alipumzisha Esaka dakika ya 82 na kuingiza Hiroto Goya katika nafasi yake.
Vijana wa Nelsinho akiwemo Olunga walipoteza nafasi kadhaa nzuri na pia watashukuru kipa Kim Seung-Gyu kwa kupangua makombora kadhaa makali kutoka kwa Cerezo.
Kiungo Mbrazil Richardson atakosa mechi mbili zijazo za Kashiwa baada ya kuonyeshwa kadi yake ya nne ya njano msimu huu dhidi ya Cerezo.
Atarejea dhidi ya FC Tokyo katika fainali ya Levain Cup mnamo Januari 4, 2021.
Baada ya mechi hiyo ya raundi ya 32, vijana wa Nelsinho wanasalia katika nafasi ya saba kwa alama 49. Wako pointi moja mbele ya Sanfrecce Hiroshima waliopoteza 1-0 dhidi ya FC Tokyo.
Mabingwa Kawasaki Frontale wanaongoza ligi hiyo ya timu 18 kwa alama 77 wakifuatiwa na Gamba Osaka (62), Nagoya Grampus (60), Cerezo (59), Kashima Antlers (55) na FC Tokyo (54) katika nafasi sita za kwanza.
Olunga anasalia juu ya jedwali la wafungaji wa mabao baada ya kutikisa nyavu mara 26. Mbrazil Everaldo anayechezea Kashima ni wa pili kwa mabao 17.