Olunga atafaulu kupiku Kipchoge tuzo za SOYA leo Ijumaa?
GEOFFREY ANENE na AYUMBA AYODI
MBIVU na mbichi kuhusu wanamichezo waliotia fora nchini Kenya mwaka 2019 itajulikana leo Ijumaa usiku wakati tuzo za SOYA zitaandaliwa mjini Mombasa.
Hakuna mwanamichezo nje ya riadha amewahi kutwaa taji la jumla tangu kitengo hiki kianzishwe mwaka 2011.
Kuwepo kwa mshikilizi wa rekodi ya dunia ya mbio za kilomita 42 Eliud Kipchoge hakutarajiwi kufanya mambo kuwa tofauti katika makala ya 16 ambayo mgeni wa heshima ni mwanasoka bora wa zamani wa Afrika Victor Ikpeba kutoka Nigeria.
Kipchoge, ambaye alishinda mataji mengi mwaka 2019 pamoja na kuibuka mwanariadha bora duniani, anawania tuzo ya mwanamichezo bora dhidi ya mshambuliaji wa Kashiwa Reysol nchini Japan Michael Olunga, bingwa mtetezi Conseslus Kipruto (mbio za mita 3,000 kuruka viunzi na maji), mshikilizi wa rekodi ya dunia ya nusu-marathon Geoffrey Kamworor na bingwa mpya wa dunia wa mbio za mita 1,500 Timothy Cheruiyot.
Bingwa wa utunishaji misuli barani Afrika Evelyne Okinyi ndiye pekee kutoka nje ya riadha katika orodha ya wawaniaji wa taji la mwanamke bora nchini.
Anakabiliwa na kibarua kigumu dhidi ya mabingwa wa dunia Hellen Obiri ambaye ni bingwa mtetezi (mita 5,000), Ruth Chepng’etich (marathon) na Beatrice Chepkoech (mita 3,000 kuruka viunzi na maji) na mshikilizi wa rekodi ya dunia ya marathon Brigid Kosgei.
Shirikisho la Mbio za Magari nchini (KMSF) linatarajiwa kuibuka shirikisho bora baada ya kurejea kwa Safari Rally katika Mbio za Magari za Dunia (WRC).
Mshambuliaji Jentrix Shikangwa anapigiwa upatu kutawala kitengo cha chipukizi bora kwa upande wa kinadada. Alisaidia Kenya kushinda mashindano ya Afrika Mashariki na Kati (Cecafa) kwa mara ya kwanza kabisa. Alifungia Harambee Starlets mabao 10 nchini Tanzania mwezi Novemba mwaka jana. Mabingwa wa michezo ya Afrika Malkia Strikers na wanaraga wa Kenya Lionesses pia hawawezi kupuuzwa.
Kitengo cha chipukizi bora kwa upande wa wavulana kinatarajiwa kunyakuliwa na mwanaraga Geoffrey Okwach ambaye aling’ara akisaidia Chipu kurejea katika Raga za Dunia (JWRT) baada ya kuwa nje miaka 10 mwaka jana. Mwanariadha Dominic Ndigiti ndiye mpinzani wake mkuu.
Kenya Morans inaonekana kuwa pazuri kuibuka bora katika kitengo cha timu ya mwaka 2019 (wanaume). Ilitikisa katika mpira wa vikapu ya AfroCan nchini Mali.
Baada ya kukosa tuzo ya Afrika, David Ouma wa Harambee Starlets huenda akawa kocha bora wa mwaka.