• Nairobi
  • Last Updated May 4th, 2024 9:55 AM
OLUNGA ATUA: Olunga akamilisha kambi ya Harambee Stars jijini Paris

OLUNGA ATUA: Olunga akamilisha kambi ya Harambee Stars jijini Paris

Na CHRIS ADUNGO

MVAMIZI Michael Olunga amekuwa mchezaji wa mwisho kutua kambini mwa Harambee Stars wanaojiandaa kwa fainali za Kombe la Afrika (AFCON) nchini Ufaransa.

Olunga aliruhusiwa na waajiri wake Kashiwa Reysol wanaoshiriki Ligi ya Daraja la Kwanza nchini Japan, kuungana na wenzake wa Stars jijini Paris baada ya Shirikisho la Soka la Kenya (FKF) kuingilia kati.

Awali, Reysol hawakuwa radhi kumwachilia Olunga ambaye walipania kumtegemea pakubwa katika mchuano wao wa mwisho wa msimu dhidi ya Ehime FC watakaokutana nao mwishoni mwa wiki hii.

Kulingana na kocha Sebestien Migne wa Stars, kucheleweshwa kwa ujio wa Olunga hadi mwanzoni mwa wiki ijayo, kungeathiri pakubwa maandalizi ya kikosi chake ambacho kina mikakati kabambe ya kumnoa vilivyo kila mchezaji.

“Kashiwa wamemwachilia Olunga hatimaye baada ya FKF kuwaandikia vinara wa Shirikisho la Soka Duniani (FIFA),” akasema Rais wa FKF, Nick Mwendwa huku akithibitisha kwamba nyota huyo alitua salama nchini Ufaransa.

Fowadi huyo wa zamani wa Thika United na Gor Mahia anatazamiwa kushirikiana vilivyo na John Avire, Masoud Juma na Christopher Mbamba katika safu ya mbele ya Stars.

Ushirikiano wao utatiwa mizanini katika mechi ya kirafiki itakayowakutanisha Stars na Madagascar jijini Paris hapo Juni 7, kisha kupigwa msasa zaidi katika mchuano mwingine wa kupimana nguvu dhidi ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo hapo Juni 15 jijini Madrid, Uhispania.

Stars ambao watapiga kambi jijini Paris hadi Juni 19, watafungua kampeni zao za Kundi C dhidi ya Algeria hapo Juni 23 kabla ya kuvaana na Tanzania siku nne baadaye.

Mchuano wao wa mwisho wa makundi utakuwa dhidi ya Senegal hapo Julai 1.

Mechi zote za Stars wanaotazamiwa kutegemea pakubwa maarifa ya wachezaji wanaosakata soka ya kulipwa katika mataifa ya kigeni, zitachezewa uwanjani 30 June jijini Cairo, Misri.

Jeraha

Mnamo Machi 2019 Olunga alikosa katika kikosi cha Stars kilichorudiana na Ghana katika mechi ya mwisho ya Kundi F ya kufuzu kwa fainali za AFCON jijini Accra baada ya waajiri wake Reysol kudai kwamba nyota huyo alikuwa akiuguza jeraha la paja.

Kulingana na Reysol wakati huo, Olunga alijeruhiwa alipokuwa akiwachezea waajiri wake dhidi ya Albirex Niigata katika kivumbi cha ligi. Aliondolewa ugani baada ya kufunga bao la pekee na la ushindi.

Tukio hilo lilimweka Migne katika ulazima wa kumwita fowadi matata wa Zesco United, Jesse Jackson Were aliyekosa kuunga orodha ya kikosi cha kwanza kilichoitwa kambini kujaza nafasi ya Olunga.

Hata hivyo, Were ambaye pia atasalia kuwa shabiki wakati wa fainali nchini Misri, alikosa kujumuishwa katika kikosi cha mwisho kilichotegemewa na Migne dhidi ya Ghana ugenini.

You can share this post!

UKUMBI WA LUGHA NA FASIHI: Dhana ya motisha ikiwemo matawi...

Familia 800 za Waislamu zapokea chakula kutoka kwa mbunge...

adminleo