Michezo

Omondi kurejelea ukocha baada ya kukosa klabu kwa miezi saba

Na CHRIS ADUNGO September 17th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

MKUFUNZI wa zamani wa Nzoia Sugar, Collins ‘Korea’ Omondi amefichua azma ya kurejelea majukumu ya ukocha msimu ujao baada ya kuwa nje kwa miezi saba.

Omondi aliagana na Nzoia mnamo Machi baada ya kikosi chake kusajili msururu wa matokeo duni yaliyowaweka katika nafasi ya 15 kwa alama 13 pekee jedwalini.

Chini ya Omondi, klabu hiyo ya Ligi Kuu ya Kenya (KPL) ilisajili ushindi mara mbili pekee, kuambulia sare mara saba na kupoteza michuano 13 kati ya 22 kwenye kampeni za msimu uliopita wa 2019-20.

Hadi alipoaminiwa fursa ya kudhibiti mikoba ya Nzoia, Omondi alikuwa kocha msaidizi wa Kariobangi Sharks. Amesema kwamba huduma zake kwa sasa zinawaniwa na vikosi viwili vya Ligi ya Kitaifa ya Supa (NSL) na akademia moja maarufu ya soka jijini Nairobi.

Hata hivyo, amesema bado anazitathmini ofa alizopokea hadi kufikia sasa kabla ya kufanya maamuzi kuhusu mahali atakapoelekea japo hakuonyesha azma ya kuendea mikoba ya akademia hiyo ambayo hakutaka kuitaja.

“Ipo akademia moja ya chipukizi na klabu mbili za NSL ambazo zimenipa ofa. Hata hivyo, nahisi kwamba nastahili kudhibiti chombo cha mojawapo ya timu za KPL,” akatanguliza.

“Nimekuwa kocha msaidizi kambini mwa Mathare United, Nairobi Stima na Sharks kabla ya kuteuliwa kuwa kocha mkuu wa Nzoia mwanzoni mwa muhula uliopita wa 2019-20.”

“Tajriba ambayo nimepata katika kipindi kizima cha kuwatia makali wanasoka wa vikosi hivyo inatosha kunifanya kocha mkuu katika klabu yoyote ya KPL kwa sasa na wala si kocha msaidizi au hata kocha wa akademia,” akaongeza kwa kusisitiza kwamba atakuwa radhi kujiunga na mojawapo ya klabu mbili za NSL zinazomhemea kabla ya kutafuta hifadhi mpya kwenye soka ya KPL kuanzia muhula wa 2021-22.

Kwa mujibu wa Omondi, uzoefu alioupata kwa kunoa kikosi cha Nzoia ulimwandaa vilivyo kukabiliana na presha ya mashabiki na usimamizi wa klabu yoyote.

Anasema kwamba changamoto zilizochangiwa na uchechefu wa fedha kambini mwa Nzoia pia zilimfunza mbinu mbalimbali za kushughulikia panda-shuka zisizokwisha katika soka ya Kenya.

“Mara nyingine kocha hujipata katika ugumu wa kuwatia motisha wanasoka kusajili matokeo ya kuridhisha wakati ambapo kikosi kinapitia hali ngumu ya kifedha. Hapa ndipo ubunifu wa kocha hutiwa kwenye mizani,” akasema Omondi ambaye kwa sasa anawatia makali chipukizi wa Korogocho Youth.