• Nairobi
  • Last Updated May 17th, 2024 7:02 PM
Onana, Pickford na Oblak, nani atajaza nafasi ya De Gea?

Onana, Pickford na Oblak, nani atajaza nafasi ya De Gea?

ANDRE Onana wa kikosi cha Ajax nchini Uholanzi, Jordan Pickford wa Everton na Jan Oblak wa Atletico Madrid wanaongoza orodha ya makipa wanaohemewa na Manchester United kwa matarajio ya kuwa mrithi wa David de Gea uwanjani Old Trafford.

Licha ya De Gea kutia saini mkataba mpya wa miaka minne na Man-United mnamo Septemba 2019, waajiri wake wamefichua mipango ya kumtema mwishoni mwa msimu huu baada ya kisu cha makali yake kusenea.

De Gea ambaye ni mzawa wa Uhispania, kwa sasa hutia kapuni kima cha Sh52 milioni kwa wiki uwanjani Old Trafford.

Kabla ya kurefusha muda wa kuhudumu kwake kambini mwa Man-United, De Gea alisuasua sana; jambo lililoibua tetesi zilizomhusisha na Juventus na Real Madrid.

Kwa mujibu wa magazeti mengi nchini Uingereza, usimamizi wa Man-United haujaridhishwa na matokeo ya De Gea tangu atie saini kandarasi mpya.

Suala hilo limechochea Man-United kutamatisha rasmi kipindi cha mkopo wa mlinda-lango Dean Henderson kambini mwa Sheffield United kwa matarajio ya kumfanya kipa chaguo la kwanza iwapo juhudi za kusajili Onana, Pickford na Oblak zitagonga ukuta.

Ingawa Man-United wako radhi kuweka mezani kima cha Sh4.9 bilioni kwa minajili ya huduma za    Onana, Edwin van der Sar ambaye ni Afisa Mkuu wa Ajax amesisitiza kwamba hawapo radhi kuzinadi huduma za kipa huyo mzawa wa Cameroon.

Mbali na Man-United vikosi vingine vinavyomvizia Onana ni Barcelona, Chelsea na Tottenham Hotpsur.

Kufikia sasa, De Gea amechezea zaidi ya mechi 400 tangu asajiliwe na aliyekuwa kocha wa klabu hiyo, Sir Alex Ferguson mnamo 2011 akitokea Atletico Madrid kwa kitita cha Sh2.4 bilioni. Ameiwajibikia timu ya taifa ya Uhispania mara 40, mbali na kuisaidia Man-United kutwaa ubingwa wa taji la EPL katika msimu wa 2012-13, Kombe la FA Cup miaka mitatu baadaye pamoja na League Cup na Europa League msimu wa 2016-17.

De Gea amekuwa akihusishwa na mpango wa kujiunga na Real Madrid mara kadhaa, na alitarajiwa kujiunga na vigogo hao wa Ligi Kuu ya Uhispania (La Liga) mapema mwaka wa 2019, lakini hakufanikiwa.

Awali, alikaribia pia kujiunga na klabu hiyo iliyokuwa tayari kutoa Sh3.7 bilioni mnamo Septemba 2015, lakini dili hiyo ikaambulia patupu.

De Gea anamezewa pia na Juventus ambao wanasaka kizibo kamili cha ‘nyani’ wa zamani wa Arsenal, Wojciech Szczesny anayehusishwa na uwezekano wa kurejea AS Roma.

You can share this post!

Mbio za Gusii Sports Legends Series zaahirishwa

Caballero kuendelea kupangua mashuti Stamford Bridge

adminleo