Ozil asema habanduki Arsenal
NA CECIL ODONGO
NYOTA wa Arsenal Mesut Ozil amefichua kwamba hana nia ya kugura klabu hiyo baada ya msimu wa 2018/19 kutamatika Jumapili Mei 12.
Ozil raia wa Ujerumani amehusishwa na uhamisho hadi klabu nyingine hasa baada ya Unai Emery kuchukua nafasi ya ukufunzi kutoka kwa Arsene Wenger mwanzo wa msimu uliokamilika.
Bodi ya Arsenal pia imeripotiwa kwamba inaridhia kuhama kwa Ozil ili kuweka akiba kitita kikubwa cha fedha anazolipwa Mjerumani huyo kila wiki kama mshahara.
Ingawa hivyo, Ozil mwenye umri wa miaka 30 amejitokeza na kupuuzilia mbali uvumi unaozingira uhamisho wake akisema anafurahia maisha ugani Emirates na katu habanduki Arsenal.
“Kwa hakika sijawazia kuihama klabu ambayo ninaihusudu sana. Bado nina miaka miwili ya kuisakatia Arsenal na kitakachofanyika baadaye hakinihusu ndewe wala sikio. Ninafurahia kuchezea klabu hii na siendi popote kwa sasa,” akasema nyota huyo aliyeongoza Ujerumani kushinda Kombe la Dunia makala ya mwaka wa 2014.
Ozil anatarajiwa kujikaza kisabuni na kuongoza Arsenal katika mechi ya fainali ya Ligi ya Uropa dhidi ya Chelsea Mei 29.
Arsenal itafuzu kwa Ligi ya Klabu Bingwa Barani Ulaya (UEFA) iwapo itafanikiwa kuibwaga Chelsea ambayo tayari imefuzu kushiriki Uefa msimu ujao wa 2019/20.