Michezo

Penalti ya Bruno Fernandes dakika ya mwisho yaimaliza Brighton

September 26th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na MASHIRIKA

PENALTI ya dakika ya mwisho katika kipindi cha pili imewapa Manchester United ushindi wa 3-2 dhidi ya Brighton uwanjani Amex,  Jumamosi na alama tatu za kwanza katika Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) msimu huu.

Mkwaju huo wa dakika ya mwisho ulifumwa wavuni na kiungo matata raia wa Ureno, Bruno Fernandes. Licha ya kwamba refa Chris Kavanagh alikuwa tayari amepuliza kipenga cha kuashiria mwisho wa mechi, teknolojia ya VAR ilibainisha kwamba fowadi Neal Maupay alikuwa amenawa mpira ndani ya kijisanduku na hivyo kuchangia tukio la Man-United kupewa penalti.

Dakika chache kabla ya kizaazaa hicho, dalili zote ziliashiria kwamba Brighton wangeridhika na alama moja kwa sare ya 2-2 kwenye mechi hiyo iliyotawaliwa na hisia kali.

Brighton walichukua uongozi kunako dakika ya 40 kupitia kwa penalti ya Maupay kabla ya Lewis Dunk kujifunga na kurejesha Man-United mchezoni dakika tatu baadaye.

Bao la Dunk liliamsha ari ya Man-United ambao walikita kambi langoni pa wenyeji wao kabla ya kufungiwa goli la pili na Marcus Rashford katika dakika ya 55. Awali, mabao mawili ya Rashford yalifutiliwa mbali na refa kwa madai kuwa alijaza mpira kimiani akiwa ameotea.

Ingawa hivyo, Brighton hawakufa moyo na waliendeleza mashambulizi ya kushtukiza mara kwa mara yaliyoshuhudia makombora matatu ya fowadi Leandro Trossard yakigonga mwamba wa goli la Man-United.

Kiu ya Brighton ya kutaka kusawazisha mambo ilizalisha penalti iliyofutiliwa mbali na VAR katika dakika ya 78 kabla ya fataki mbili za Maupay kugonga mchuma wa lango la kikosi cha kocha Ole Gunnar Solskjaer.

Ilikuwa hadi dakika ya 95 ambapo Brighton walisawazishiwa na Solly March aliyekamilisha krosi ya Alireza Jahanbakhsh kwa kichwa.

Man-United walijibwaga ugani kwa minajili ya mchuano huo wakiwa na ulazima wa kujinyanyua baada ya chombo chao kuzamishwa kwa kichapo cha 3-1 kutoka kwa Crystal Palace katika mechi ya ufunguzi wa msimu huu ugani Old Trafford.

Brighton nao walikuwa na motisha ya kuendeleza ubabe uliowashuhudia wakiwapepeta Newcastle 3-0 wikendi iliyopita ugani St James’ Park.

Hata hivyo, hamasa kutoka kwa pande zote ilitarajiwa hasa baada ya Man-United kucharaza Luton 3-0 nao Brighton kuipiga Preston 2-0 kwenye mechi zilizozipta za Kombe la Carabao.

Hadi kufikia jana, Man-United walikuwa pia wakijivunia rekodi nzuri dhidi ya Brighton ambao walichapa 3-0 ugani Amex kwa mara ya mwisho mnamo Juni 30.

Awali, masogora wa Man-United walikuwa wamepoteza mara mbili mfululizo dhidi ya Brighton uwanjani Amex mnamo 2018-19. Man-United kwa sasa wanajiandaa kwa ratiba ngumu itakayowakutanisha na Tottenham Hotspur, Chelsea na Arsenal kwenye msururu wa mechi nne zijazo.