Michezo

Pigo kwa Gor wachezaji 4 muhimu kukosa mechi ya Berkane

March 29th, 2019 Kusoma ni dakika: 1

Na GEOFFREY ANENE

MABINGWA wa Kenya, Gor Mahia watakosa huduma muhimu za wachezaji Haron Shakava, Shafik Batambuze, Jacques Tuyisenge na Ernest Wendo watakapomenyana na Berkane kutoka Morocco kwenye robo-fainali ya Kombe la Mashirikisho mwezi April 2019.

Beki Shakava atakosa mchuano wa Aprili 7 pekee kwa sababu ya kuonyeshwa kadi mbili za njano katika mechi mbili tofauti za mashindano haya.

Kiungo Batambuze kutoka Uganda atakuwa shabiki Gor itakapomenyana na Berkane uwanjani Kasarani mnamo Aprili 7 pamoja na kukosa mechi ya marudiano nchini Morocco mnamo Aprili 14.

Alikula kadi mbili za njano katika mechi mbili tofauti na kutumikia marufuku ya mechi moja, lakini sasa atakuwa nje mechi mbili kwa sababu kuonyeshwa kadi mbili za njano katika mechi moja.

Mshambuliaji matata wa Rwanda, Tuyisenge pia hatakuwepo kwa mechi dhidi ya Berkane nyumbani na ugenini kwa sababu alikuwa ameonyeshwa kadi ya njano katika mechi mbili tofauti na kufuatiwa na kadi zingine mbili za njano katika mechi mbili tofauti ikiwemo kuadhibiwa kwa kutumia mbinu ya kuchelewesha mechi kuendelea.

Mabao

Tuyisenge anaongoza kufungia Gor mabao katika mashindano haya ya daraja ya pili ya Afrika akiwa ameona lango katika mechi tano zilizopita dhidi ya Petro de Luanda (Angola), Hussein Dey (Algeria), Zamalek (Misri), New Star (Cameroon) na Lobi Stars (Nigeria) jijini Nairobi.

Wendo atakosa mechi tatu zijazo za Gor baada ya kuonyeshwa kadi mbili za njano katika mechi mbili tofauti na kulishwa kadi nyekundu katika mechi iliyopita dhidi ya Petro kwa kuchezea mpinzani vibaya sana.

Kipa Frederick Odhiambo, ambaye alionyeshwa kadi ya njano dhidi ya Petro jijini Nairobi kwa tabia isiyo ya kispoti, aliponea adhabu kutoka kwa Shirikisho la Soka barani Afrika (CAF).