• Nairobi
  • Last Updated May 3rd, 2024 3:16 PM
Pochettino asema haogopi kupigwa kalamu na Tottenham Hotspur

Pochettino asema haogopi kupigwa kalamu na Tottenham Hotspur

Na MASHIRIKA

LONDON, UINGEREZA

KOCHA Mauricio Pochettino amesema haogopi kutimuliwa na usimamizi wa Tottenham Hotspur kutokana na msururu wa matokeo duni ya kikosi chake.

Spurs walipokezwa na Brighton kichapo cha 3-0 mnamo Jumamosi katika mchuano wa Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) uliowakutanisha uwanjani American Community Express.

Kichapo hicho kilijiri siku chache baada ya Spurs kunyeshewa 7-2 na Bayern Munich katika kivumbi cha Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) mbele ya mashabiki wao wa nyumbani jijini London, Uingereza.

Awali, Tottenham walikuwa wamebanduliwa na limbukeni Colchester wanaoshiriki Ligi ya Daraja ya Pili nchini Uingereza kwenye kampeni za kuwania ufalme wa Carabao Cup. Alipoulizwa iwapo matokeo mabovu ya vijana wake yanamhofisha, Pochettino alisisitiza kwamba hakuna chochote kinachompigisha mshipa.

“Sina hofu wala shaka. Kinachostahili kunihangaisha ni maisha, si mpira,” akatanguliza kocha huyo mzawa wa Argentina.

“Soka ni mchezo ambao mara nyingine utashinda au kupoteza. Tatizo lililopo kwa sasa Tottenham ni kwamba kocha na wachezaji wamewekwa katika ulazima wa kusajili ushindi katika takriban kila mchuano. Hili ni jambo lisilowezekana,” akasema Pochettino.

Kichapo cha hivi karibuni zaidi cha Tottenham waliokuwa wanafainali ya Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) miezi minne iliyopita ina maana kwamba wamejizolea alama 11 pekee kutoka kwa jumla ya pointi 24 walizokuwa katika uwezo wa kujitwalia.

Chini ya Pochettino, Tottenham wameshindwa kabisa kusajili ushindi katika michuano 10 iliyopita ya EPL ugenini. Mechi yao ya mwisho kushinda ni kibarua kilichowakutanisha na Fulham na kumalizika kwa 2-0 ugani Craven Cottage mnamo Januari 20, 2019.

Kwa ujumla, Tottenham wamepoteza mechi 17 hadi kufikia sasa katika michuano yote ya msimu huu.

Kwa mujibu wa magazeti mengi nchini Uingereza, huenda hali tete inayowakabili Tottenham kwa sasa imechangiwa na utata kuhusu mustakabali wa nyota Christian Eriksen, Toby Alderweireld na Jan Vertonghen ambao wamesalia na mwaka mmoja pekee katika mikataba yao na miamba hao wa soka ya Uingereza.

Baada ya kudhalilishwa 7-2 na Bayern katika kivumbi cha UEFA, yalikuwa matarajio ya Pochettino kwamba vijana wake wangalijinyanyua dhidi ya Brighton na kuwekea dira kampeni zao za muhula huu.

Ushindi wa 2-1 uliosajiliwa na Tottenham dhidi ya Southampton uliwapa vijana wa Pochettino afueni tele siku chache baada ya Colchester kuwadengua kwenye kivumbi cha Carabao Cup.

Kichapo cha jana kinatarajiwa sasa kumning’iniza padogo zaidi Pochettino.

Mwishoni mwa wiki jana, Spurs walifichua mipango ya kumpokeza kocha Gareth Southgate wa timu ya taifa ya Uingereza mikoba yao iwapo Pochettino atatimuliwa.

Fainali ya msimu jana

Kocha huyo mzawa wa Argentina tayari ameanza kuhusishwa na uwezekano mkubwa wa kutua kambini mwa Manchester United iwapo atahiari kuagana na Tottenham waliokuwa wanafainali wa UEFA msimu jana.

Itakuwa ni mara ya pili kwa Tottenham kuziwania huduma za Southgate, 49, hasa ikizingatiwa kwamba waliwahi kuyataka maarifa ya mkufunzi huyo kwa mara nyingine mwishoni mwa msimu uliopita. Hatua hiyo ilichochewa na suitafahamu kuhusu mustakabali wa Pochettino aliyekuwa akiandamwa sana na Real Madrid huku naye akisitasita kusalia Tottenham kwa mwaka wa tano.

Kabla ya kuwaongoza vijana wake kumenyana na Liverpool kwenye fainali ya UEFA msimu uliopita, Pochettino alikiri kwamba alikuwa radhi kuondoka Tottenham iwapo masogora wake wangaliwazidi Liverpool maarifa. Nusura matamshi hayo ya Pochettino ambaye amesisitiza kuwa ndiye anayestahili kulaumiwa kwa masaibu ya kikosi chake, yasambaratishe Tottenham huku baadhi ya wachezaji wakifichua maazimio ya kubanduka.

You can share this post!

Pogba ataka Manchester United wamlipe Sh78m kwa wiki

ADUNGO: Tusidanganyane, ligi kuu msimu huu ni ya farasi 2;...

adminleo