Pogba alilia ruhusa ya kuhama Manchester United
Na MASHIRIKA
MANCHESTER, Uingereza
KIUNGO Mfaransa, Paul Pogba amesema wakati wake wa kuagana na Manchester United umefika, na hakuna atakayemzuia kuondoka.
Nyota huyo mwenye umri wa miaka 26 ambaye aliisaidia timu ya taifa – Ufaransa – kutwaa ubingwa wa Kombe la Dunia alisema, “Wakati wangu wa kuhamia kwingine umetimia.”
Pogba amehusishwa na mpango wa kuhamia Real Madrid au kurejea Juventus; zinazotamani kumnunua staa huyo kwa kitita kikubwa kuliko anachopokea uwanjani Old Trafford na tayari amewajulisha mabosi wake wa United wamuachilie.
Madrid wanapanga kufanya usajili wa nguvu, lakini tatizo ni jinsi watakavyodumisha usawa wa kifedha (FFP).
Hii ni baada ya uchanganuzi wa hesabu za klabu hizo kuashiria kwamba wana uwezo mkubwa wa kutumia hela zaidi.
Mbali na kumsajili kipa Thibauti Courtois kutoka Chelsea msimu uliopita, Madrid wamejiepusha na majina makubwa tangu 2014, wakati mastaa walipojiunga na klabu hiyo wakiwemo Toni Kroos na James Rodriguez.
Madrid wametumia karibu Sh45 bilioni tangu mwisho wa msimu uliopita, ambapo ilidaiwa walivunja rekodi kwa kutumia Sh34 bilioni mnamo 2009 waliposajili majina makubwa -Cristiano Ronaldo, Karim Benzema, Kaka na Xavi Alonso.
Wakati huu wakiwania saini ya Pogba, tayari vigogo hao wa La Liga wamemsajili Eden Hazard kutoka Chelsea kwa Sh15 bilioni.
Mshambuliaji Luka Jovic wa Serbia naye alisajiliwa kutoka Eintracht Frankfurt ya Ujerumani kwa Sh8 bilioni, na pia wamemtwaa beki matata wa kushoto Ferland Mendy kutoka Lyon ambaye mkataba wake uligharimu Sh7 bilioni.
Mlinzi Eder Militao wa Porto naye ameingia Bernabeu kwa Sh7.2 bilioni pamoja na mshambuliaji matata Rodrygo, 18 wa Brazil. Kina huyo alinunuliwa kwa Sh6 bilioni akitokea Santos.
Utafiti uliofanyiwa akaunti zake majuzi ulionyesha kwamba klabu hiyo ya Uhispania ilikuwa na pato la Sh75 bilioni, licha ya kuondolewa mapema katika michuano ya Klabu Bingwa barani Ulaya (UEFA) msimu wa 2018-19.
Mapato
Ufanisi wao ulitokana na mapato ya mechi za kirafiki pamoja na mauzo ya kibiashara na huenda zikafidia pengo lililopo.
Kadhalika, Madrid wananufaika kutokana na mabadiliko katika mfumo wa kuhesabu pesa zinazolipwa na klabu ambazo hadi msimu wa 2018-19 zimekuwa zikifanya vizuri dhidi ya timu nyingine kwa misimu 10 iliyopita katika michuano ya Klabu Bingwa na Europa League.
Madrid imetumia fedha nyingi msimu huu, lakini pia ilipokea mabilioni baada ya kumuuza Ronaldo kujiunga na Juventus, pesa ambazo zitaingia kwenye akaunti yake msimu wa 2018-19.
Kwa mujibu wa taarifa zilizochapishwa mwezi Juni 2018, Real Madrid ilikuwa na Sh28.5 bilioni katika benki yake.