Prisons yaingia 8-bora na kubeba matumaini ya Kenya kupata medali voliboli ya Klabu Bingwa Afrika ya wanaume
Na GEOFFREY ANENE
KENYA Prisons itamenyana na Smouha katika mechi ya robo-fainali ya Klabu Bingwa Afrika ya voliboli ya wanaume baada ya kujikatia tiketi kwa kunyuka Rukinzo kutoka Burundi kwa seti 3-0 jijini Cairo, Misri, Jumamosi.
Vijana wa kocha David Lung’aho walihitaji ushindi pekee kuingia mduara wa nane-bora na hawakusikistisha, wakilemea Espoir kwa alama 25-16, 25-7, 25-21.
Wakenya hawa, ambao walishinda medali ya fedha katika mashindano haya mwaka 2011, wanaungana na Nemo Stars (Uganda), Asaria, Etihad na Swehly (Libya) na Smouha na mabingwa watetezi Al Ahly (Misri).
Nemo Stars imeshangaza wengi. Baada ya kushindwa kufika robo-fainali miaka sita, Waganda hao walitinga robo-fainali kwa kucharaza wapinzani wake wote wa Kundi D wakiwemo mabingwa wa Kenya, General Service Unit, ambao mwaka huu wametupwa katika mduara wa kuwania nafasi ya 9-16.
Prisons sasa itakabiliana na Smouha katika mechi ya robo-fainali. Klabu za GSU na Prisons zilikuwa zimeapa kabla ya mashindano kuleta taji nchini Kenya. Kwa sasa, matumaini yote ya Kenya kuandikisha historia ya kuwa timu ya kwanza nje ya kaskazini mwa Afrika kutwaa taji yako mikononi mwa Prisons.