PSG na Basaksehir kurudiana baada ya mechi ya Jumanne kuvurugwa na tukio la ubaguzi wa rangi
Na MASHIRIKA
MECHI ya Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) kati ya Paris Saint-Germain (PSG) na Istanbul Basaksehir sasa itaendelezwa usiku wa Disemba 9, 2020, baada ya mchuano huo ulioratibiwa kuchezwa Disemba 8, 2020 kufutiliwa mbali baada ya afisa mmoja wa mechi kutuhumiwa kutumia matamshi ya kuashiria ubaguzi wa rangi.
Kwa mujibu wa Istanbul, msaidizi wa refa, Sebastian Coltescu alitumia matamshi yenye kuashiria ubaguzi wa rangi dhidi ya kocha msaidizi, Pierre Webo.
Webo ambaye ni mwanasoka wa zamani wa Cameroon, alionyeshwa kadi nyekundu wakati wa mchuano huo kwa kuzozana na Coltescu.
Hatua hiyo ilichochea wachezaji wa Basaksehir kuondoka uwanjani wakilalamikia tukio hilo la ubaguzi wa rangi nao wakafutwa na wanasoka wa PSG.
Tukio hilo lilifanyika katika dakika ya 14, vikosi vyote viwili kwenye mechi hiyo ya Kundi H vikiwa bado havijafungana bao.
Kwa mujibu wa waandalizi, mchuano huo utaendelezwa sasa mnamo Disemba 8, 2020 kuanzia saa nne kasoro dakika tano (9:55pm) uwanjani Parc des Princes jijini Paris, Ufaransa.
Maafisa wapya watakaoongozwa na Danny Makkelie wa Uholanzi atasimamia mchuano huo. Wasaidizi wake watakuwa Mario Diks wa Uholanzi pamoja na Marcin Boniek na Bartosch Frankowsky kutoka Poland.
PSG tayari wamefuzu kwa hatua ya 16-bora ya UEFA baada ya washindani wao wengine katika Kundi H, Manchester United kupokezwa kichapo cha 3-2 kutoka kwa RB Leipzig ya Ujerumani.