PSG yaipepeta Rennes 3-0 ligini
Na MASHIRIKA
ANGEL Di Maria alifunga mabao mawili naye Moise Kean akapachika wavuni bao lake la tano kutokana na mechi tano kambini mwa Paris Saint-Germain (PSG) mnamo Novemba 7, 2020.
Mabao ya wanasoka hao yalisaidia waajiri wao PSG kupepeta nambari tatu Rennes 3-0 kwenye Ligi Kuu ya Ufaransa (Ligue 1) na kufungua pengo la alama tano kileleni mwa jedwali.
Hata hivyo, raha ya PSG kutokana na ushindi huo iliyeyushwa na majeraha mabaya ambayo huenda yakawaweka nje kwa muda mrefu wanasoka Kean, Thilo Kehrer na Idrissa Gueye. Watatu hao walilazimika kuondoka uwanjani kabla ya mechi dhidi ya Rennes kukamilika.
Kean aliwaweka PSG uongozini katika dakika ya 11 kabla ya Di Maria kufunga magoli mengine mawili kunako dakika za 21 na 73.
Rennes ambao kwa sasa wananolewa na kocha Julien Stephan walitatiza pia mabeki wa PSG mara kwa mara na kumweka kipa Keylor Navas katika ulazima wa kufanya kazi ya ziada.
Kocha Thomas Tuchel aliwaongoza masogora wake wa PSG kunogesha mchuano huo dhidi ya Rennes bila ya huduma za wanasoka Kylian Mbappe, Neymar, Juan Bernat, Mauro Icardi, Presnel Kimpembe, Julian Draxler, Pablo Sarabia na Marco Verratti ambao wanauguza majeraha.
Tuchel alilazimika kujaza mapengo yaliyoachwa na Gueye na Kehrer katika kipindi cha kwanza kabla ya Kean kuondoka uwanjani akichechemea mwanzoni mwa kipindi cha pili. Beki Alessandro Florenzi wa PSG pia alipata jeraha kwenye mchuano huo.