Raia wa Urusi aliyejitapa hatumii pufya afeli vipimo kwenye Olimpiki
Na GEOFFREY ANENE
MWANAMICHEZO Nadezhda Sergeeva aliyejigamba hatumii dawa za kusisimua misuli amefeli vipimo vya matumizi ya dawa hizo haramu.
Kwa mujibu wa tovuti ya Huff Post, raia huyo wa Urusi, ambaye anashiriki fani ya bobsled alionekana kwenye video katika mtandao wa Instagram mnamo Februari 15 akivalia tishati iliyokuwa na maandishi “I Don’t Do Doping (Mimi situmii dawa za kusisimua misuli).”
Siku tatu baadaye, Sergeeva alipatikana na kosa la kutumia dawa zilizopigwa marufuku kwenye Olimpiki za msimu wa baridi mjini Pyeongchang nchini Korea Kusini.
Alikataa kwamba alitumia dawa zilizomfanya afeli vipimo hivyo. Mnamo Februari 18, Sergeeva, ambaye alimaliza katika nafasi ya 12 katika kitengo cha bobsleigh cha wachezaji wawili wanawake, alipatikana ametumia dawa ya kutibu ugonjwa wa angina iliyokuwa na dawa za kumfanya awe bora kuliko wapinzani wenzake.
Siku tano kabla ya kufeli vipimo hivyo, Sergeeva hakuwa amepatikana na kosa hilo. Alisema hakutumia dawa hizo. Rais wa mchezo huo nchini Urusi, Alexander Zubkov alisema mwanamichezo huyo hakuambiwa atumie dawa zozote kwa matibabu.