Michezo

Rais aadhibiwa na FIFA kuchochea mashabiki kuchoma jezi ya Messi

August 27th, 2018 Kusoma ni dakika: 1

Na GEOFFREY ANENE

SHIRIKISHO la Soka Duniani (FIFA) limepiga marufuku Rais wa Soka wa Palestina (PFA) Jibril Rajoub kuhudhuria mechi miezi 12 na kumtoza faini ya Sh2,049,295 kwa kuchochea chuki na ghasia dhidi ya mwanasoka shupavu Lionel Messi.

Rajoub, ambaye pia ni Rais wa Kamati ya Olimpiki ya Palestina, aliambia mashabiki nchini mwake wachome picha na jezi zinazoonyesha supasta huyu wa Argentina akiamua kushiriki mechi ya kirafiki dhidi ya Israel mjini Jerusalem mnamo Juni 9, 2018.

Uchochezi huo ulisukuma Argentina kuvunjilia mbali ziara yake nchini Israel licha ya Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu kuomba mwenzake kutoka Argentina, Mauricio Macri, kwamba mechi hiyo iendelee.

Matamshi ya uchochezi ya Rajoub yalimfanya amulikwe na Kamati ya Nidhamu ya FIFA.

Rajoub alianza kutumikia marufuku hiyo Agosti 24, 2018. Hataweza kuhudhuria mechi ama mashindano yoyote kama kiongozi wa soka. Argentina ililenga kutumia mechi dhidi ya Israel kujipima nguvu kabla ya kuelekea nchini Urusi kwa Kombe la Dunia lililofanyika Juni 14 hadi Julai 15, 2018.

Argentina ilibanduliwa nje na Ufaransa katika raundi ya 16-bora kwa kulazwa 4-3 Juni 30. Ufaransa ilizaba Uruguay 2-0 katika robo-fainali, ikalemea Ubelgiji 1-0 katika nusu-fainali kabla ya kuibuka bingwa kwa kunyuka Croatia 4-2 katika fainali.