Rais wa Barcelona ana 'uhakika' Messi atastaafu soka akivalia jezi za klabu hiyo
Na CHRIS ADUNGO
RAIS wa Barcelona, Josep Maria Bartomeu amesema “hana shaka kabisa” kwamba fowadi na nahodha wao matata mzawa wa Argentina, Lionel Messi atatia saini mkataba mpya atakaopokezwa na miamba hao wa soka ya Uhispania (La Liga).
Mkataba kati ya Barcelona na Messi, 33, unatarajiwa kutamatika rasmi mwishoni mwa 2021 na sogora huyo aliibua tetesi kuhusu uwezekano wa kubanduka kwake uwanjani Camp Nou mwanzoni mwa Julai baada ya kukiri “kuchoshwa” na Barcelona.
“Messi amesema mara nyingi kwamba kubwa zaidi katika matamanio yake ni kustaafu akivalia jezi za Barcelona. Sina shaka kwamba atarefusha kipindi cha kuhudumu kwake ugani Camp Nou,” akasema Bartomeu katika mahojiano yake na gazeti la Mundo Deportivo.
Barcelona walikamilisha kampeni zao za Ligi Kuu ya Uhispania (La Liga) msimu huu katika nafas ya pili kwa alama tano nyuma ya mabingwa Real Madrid.
Kwa sasa wanajiandaa kurudiana na Napoli katika hatua ya 16-bora ya Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) mnamo Agosti 8, 2020 uwanjani Camp Nou. Watajibwaga ugani kwa minajili ya gozi hilo wakijivunia sare ya 1-1 waliyosajili ugenini Italia mnamo Februari 2020.
Messi ambaye alitawazwa Mfungaji Bora wa La Liga kwa mabao 25 mwishoni mwa msimu wa 2019-20 aliwahi pia kunukuliwa na Mundo Deportivo akisisitiza kwamba “italazimu mambo kubadilika na mizozo ya mara kwa mara kati ya wachezaji wazoefu, wasimamizi wa klabu ba benchi ya kiufundi kukoma iwapo Barcelona watataka kurejea katika uthabiti wao wa zamani.”
Bartomeu pia amefichua uwezekano wa Barcelona kusajili wachezaji wanne wakiwemo Miralem Pjanic (Juventus) na Lautaro Martinez (Inter Milan) huku wakiwatia mnadani wanasoka wanane mwishoni mwa msimu huu wakiwemo Rafinha, Ivan Rakitic, Arturo Vidal, Nelson Semedo, Junior Firpo, Todibo, Arthur Melo na Samuel Umtiti anayehusishwa pakubwa na Arsenal na Manchester United.