Ratcliffe aonyesha kukosa imani na Ten Hag
MMILIKI mwenza wa klabu ya Manchester United Sir Jim Ratcliffe amekataa kumpa hakikisho Erik ten Hag kuhusu kuendelea kuwa kocha mkuu wa the Red Devils.
Tetesi sasa zinasema kuwa Mholanzi huyo anaweza kufutwa kazi wakati timu za taifa zitakuwa viwanjani ligi ikiwa mapumzikoni Oktoba 7-15.
Mmiliki wa kampuni ya INEOS, Ratcliffe alichukua jukumu la kuongoza operesheni za soka ugani Old Trafford mwezi Februari 2024 baada ya kununua asilimia 25 ya hisa za klabu hiyo katika mpango uliogharimu Sh219.7 bilioni (Pauni za Uingereza 1.3 bilioni).
Viongozi wa INEOS waliamua kumuunga mkono Ten Hag mwisho wa msimu 2023-2024 licha ya klabu hiyo kukamata nafasi ya nane kwenye Ligi Kuu ya Kandanda Uingereza.
Japo United ilitafuta makocha wanaoweza kuchukua nafasi ya Ten Hag na hata kuhoji baadhi yao, uamuzi ulifanywa wa kuweka imani katika kocha huyo wa zamani wa Ajax.
United pia walimwongezea Ten Hag kandarasi hadi mwaka 2026 baada ya timu yake kutwaa ubingwa wa Kombe la FA na kuingia Ligi ya Europa.
Hata hivyo, uamuzi wa kumkwamilia Ten Hag unaonekana umerejea kuwafanya wajute kwani United wanahangaika msimu 2024-2025.
Mashetani hao wekundu wanashikilia nafasi ya 13 ligini na nambari 21 kwenye Uropa bila ya kupata ushindi katika michuano minne mfululizo. Walitoka 3-3 dhidi ya wenyeji Porto nchini Ureno mnamo Oktoba 3 usiku.
Matokeo hayo yameongeza uvumi kuwa Ten Hag ataachishwa kazi vijana wake wakipoteza dhidi ya Aston Villa kwenye Ligi Kuu hapo Oktoba 6.
Alipoulizwa na shirika la habari la BBC iwapo bado ana imani na Ten Hag, Ratcliffe alisema aliunga mkono Mholanzi huyo, lakini akaongeza kuwa uamuzi kuhusu Ten Hag kuwa kocha ugani Old Trafford si wake kufanya.
“Sitaki kujibu swali hilo… Napenda Erik. Nadhani ni kocha mzuri sana, lakini mwisho wa siku si mimi wa kufanya uamuzi, ni wasimamizi wa timu wanaoendesha Manchester United ambao wataamua njia gani nzuri ya kuendesha timu katika njia nyingi tofauti,” akasema Ratcliffe.
“Lakini timu hiyo inayoendesha Manchester United imekuwa pamoja tangu Juni ama Julai. Hawakuwepo Januari, Februari, Machi ama Aprili,” akasema Ratcliffe kuhusu Afisa Mkuu Mtendaji Omar Berrada, Mkurugenzi wa Michezo Dan Ashworth waliowasili Julai.
“Hawajakuwa hapa kwa muda mrefu kwa hivyo tunahitaji kuangalia kikosi chetu na kufanya uamuzi wa busara. Lengo letu liko wazi – tunataka kurejesha Manchester United ambako inafaa kuwa na ukweli ni kuwa bado hatajufaulu,” akasema Muingereza huyo.
Baada ya kugawana alama na Porto, Ten Hag alitaka watu wawe na subira naye na wachezaji wake.
“Sote tuko katika hali moja, wamiliki, viongozi wa timu, wafanyakazi,” akasema.
“Niliteua wafanyakazi wapya. Tulinunua wachezaji wapya chipukizi na ni muhimu kuwapa nafasi, akiwemo Manuel Ugarte. Najua kuwa katika taaluma ya kandanda mtu huwa hapewi muda. Wanafaa kuanza kuonyesha matokeo mara moja, ingawa hiyo sio hali halisi. Ugarte lazima apate kuzoea mfumo wetu, wachezaji wenzake, makali ya Ligi Kuu ya Uingereza. Hivi ni vitu vinahitaji muda,” akasema Ten Hag.
-Imetafsiriwa na Geoffrey Anene