RB Leipzig yatupa Manchester United nje ya UEFA kwenye hatua ya makundi
Na MASHIRIKA
MANCHESTER United walibanduliwa kwenye hatua ya makundi ya Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) msimu huu baada ya kupokezwa kichapo cha 3-2 kutoka kwa RB Leipzig ya Ujerumani katika mchuano wa mwisho wa Kundi H mnamo Disemba 8, 2020.
Chini ya kocha Ole Gunnar Solskjaer, Man-United walishuka dimbani wakilenga kusajili sare ya aina yoyote dhidi ya wenyeji wao ili kusonga mbele kwenye kampeni za UEFA muhula huu.
Hata hivyo, walijipata chini kwa mabao mawili katika dakika 13 za ufunguzi wa kipindi cha kwanza kabla ya Leipzig kufungiwa goli la tatu katika dakika ya 70.
Ingawa bao la penalti kutoka kwa Bruno Fernandes na jingine kutoka kwa Paul Pogba yalipania kurejesha Man-United mchezoni katika kipindi cha pili, Leipzig walisalia thabiti katika safu yao ya ulinzi.
Angelino ambaye aliwafungulia Leipzig ukurasa wa mabao katika dakika ya pili kabla ya kuchangia jingine katika dakika ya 13, ni mwanasoka wa Manchester City ambaye kwa sasa anacheza soka nchini Ujerumani kwa mkopo.
Mambo yangalikuwa mabaya zaidi kwa Man-United kufikia mwisho wa kipindi cha kwanza ambapo bao la tatu la Leipzig lilikataliwa kwa mabao kwamba kiungo Willi Orban alicheka na nyavu akiwa ameotea.
Penalti ambayo Man-United walipata katika kipindi cha pili ilikuwa zao la kuchezewa visivyo kwa Mason Greenwood aliyeangushwa na Ibrahima Konate ndani ya kijisanduku.
Kubanduliwa kwa Man-United kwenye gozi la UEFA sasa kunawashusha hadi Europa League, kipute walichokitawala mnamo 2017 na kuibuka mabingwa.
Leipzig wanatinga hatua ya 16-bora ya UEFA kwa mara ya pili mfululizo baada ya kubanduliwa kwenye nusu-fainali za msimu wa 2019-20.
Miamba hao wa soka ya Ujerumani kwa sasa wanasubiri matokeo ya marudio ya mechi kati ya Paris Saint-Germain (PSG) na Istanbul Basaksehir ili kubaini iwapo wanakamilisha kampeni za Kundi H kileleni au katika nafasi ya pili.
Man-United walianza kampeni zao za UEFA msimu huu wakipigiwa upatu wa kuibuka kileleni mwa Kundi H baada ya kuwapiga PSG 2-1 ugenini na kuwapokeza Leipzig kichapo cha 5-0 uwanjani Old Trafford katika michuano ya mikondo ya kwanza.
Masogora hao wa Solskjaer wanajiandaa sasa kuvaana na Manchester City katika gozi kali la Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) litakalosakatiwa uwanjani Old Trafford mnamo Disemba 12, 2020.