Real Madrid yatoka nyuma na kulaza Betis katika mechi ya La Liga
Na MASHIRIKA
REAL Madrid walitoka nyuma na kulaza Real Betis 3-2 katika mchuano wa Ligi Kuu ya Uhispania (La Liga) ulioshuhudia matukio mengi uwanjani yakithibitishwa na marefa kupitia teknolojia ya VAR.
Federico Valverde aliwaweka Madrid kifua mbele katika dakika ya 14 kabla ya Aissa Mandi kusawazishia wenyeji katika dakika ya 35.
William Carvalho aliwaweka Betis uongozini dakika mbili baadaye.
Emerson Leite de Souza Junior alijifunga katika dakika ya 48 na kuwapa Madrid motisha ya kurejea mchezoni na kuwatamalaki katika takriban kila idara.
Presha kutoka kwa Madrid ilichangia Emerson kumkabili kiungo Luka Modric vibaya na hivyo akaonyeshwa kadi nyekundu katika dakika ya 67.
Beki na nahodha Sergio Ramos aliwafungia Madrid bao la ushindi kupitia penalti ya dakika 82.
Maamuzi ya kuwapa Madrid penalti hiyo yalichukua muda mrefu baada ya refa kutaka kuthibitisha kupitia VAR iwapo beki Marc Bartra wa Betis alikuwa amenawa mpira uliokuwa umepigwa na Borja Mayoral ndani ya kijisanduku.
Ushindi huo ulikuwa wa kwanza kwa Madrid walioanza kampeni za kutetea ubingwa wa La Liga msimu huu kwa sare tasa dhidi ya Real Sociedad mnamo Septemba 20, 2020.
Barcelona ambao ni washindani wakuu wa Madrid, walianza kampeni za muhula huu kwa kuvaana na Villarreal mnamo Septemba 27 uwanjani Camp Nou.