Rekodi ya dunia ya Rudisha, Chepkoech hatarini Brussels Diamond League
MACHO yatakuwa kwa rekodi za dunia za watimkaji David Rudisha, Beatrice Chepkoech na Muethiopia Gudaf Tsegay ambazo zitalengwa kuvunjwa wakati wa duru ya mwisho ya riadha za Diamond League mjini Brussels, Ubelgiji hapo Septemba 13 na 14.
Rekodi ya 800m ya wanaume ya 1:40.91 iliwekwa na Rudisha mnamo Agosti 9, 2012 kwenye Olimpiki mjini London, Uingereza.
Bingwa mpya wa Olimpiki, Emmanuel Wanyonyi alikosa rekodi hiyo pembamba akishinda Lausanne Diamond League kwa 1:41.11.
Wanyonyi anayetetea taji la Diamond League baada ya kulinyakua mwaka 2023, anatarajiwa kupata ushindani mkali kutoka kwa bingwa wa dunia Marco Arop wa Canada (1:41.20) pamoja na Djamel Sedjati kutoka Algeria (1:41.46) na Mfaransa Gabriel Tual (1:41.61).
Mzawa wa Kenya, Winfred Yavi, ambaye anawakilisha Bahrain kimataifa, naye alikaribia sana rekodi ya dunia ya Chepkoech katika 3,000m kuruka viunzi na maji baada ya kutawala duru ya Roma kwa 8:44.39 nchini Italia mnamo Agosti 31. Alikosa rekodi hiyo kwa sekunde 0.07.
Bingwa huyo wa dunia na Olimpiki yuko katika orodha ya washiriki wa Brussels ambayo pia ina bingwa wa Olimpiki mwaka 2020, Peruth Chemutai kutoka Uganda (8:48.03) na chipukizi Faith Cherotich (8:55.15).
Chemutai na Cherotich waliridhika na fedha na shaba kwenye Olimpiki za 2024 mwezi Agosti nchini Ufaransa.
Chepkoech ameshikilia rekodi ya 3,000m kuruka viunzi na kinadada tangu Julai 20, 2018. Aliiweka mjini Monaco.
Naye, malkia wa dunia mbio za nyika na kilomita tano barabarani Chebet, ambaye alitwaa dhahabu kwenye Olimpiki katika 5,000m na 10,000m mwezi Agosti, alikosa rekodi ya dunia ya 5,000m ya 14:00.21 ya Tsegay kwa sekunde 9.31 akitawala Zurich Diamond League.
Chebet alisema majuzi kuwa bado ana ndoto ya kuvunja rekodi hiyo iwe ni mwaka huu ama ujao.
Tsegay alifyatuka 14:00.21 mnamo Septemba 17, 2023 kwenye Eugene Diamond League nchini Amerika.