Reynold Kipkorir kivutio mbio za nyika za Nairobi Oktoba 10
NYOTA Reynold Cheruiyot Kipkorir atakuwa kivutio kikuu katika Mbio za Nyika za Shirikisho la Riadha Kenya (AK) tawi la Nairobi, yatakayofanyika katika Uwanja wa Kimataifa wa Moi, Kasarani hapo Oktoba 10, 2025.
Kipkorir, ambaye hivi majuzi alishinda medali ya shaba katika mbio za mita 1,500 kwenye Riadha za Dunia nchini Japan, atashiriki katika mbio za kilomita mbili kwenye mashindano hayo ambayo yamevutia zaidi ya wanariadha 5,000.
Bingwa huyo wa dunia wa chipukizi wasiozidi umri wa miaka 20 mwaka 2022 na bingwa wa Afrika wa chini ya miaka 20 mwaka 2023 katika mbio za 1,500m, analenga kuchaguliwa katika timu ya Nairobi kwa ajili ya Mbio za Nyika za Kitaifa zitakazofanyika Oktoba 25 mjini Eldoret. Ni mjini Eldoret ambapo AK itateua Timu ya Kenya itakayoshiriki Mbio za Nyika za Dunia mnamo Januari 10, 2026 mjini Tallahassee, Florida, Amerika.
Kipkorir ana nia ya kuongoza tena timu mseto ya kupokezana vijiti ya Kenya kutetea taji lao kwa mara ya tatu mfululizo nchini Amerika.
“Nitafurahi nikifanikiwa kuingia tena kwenye Timu ya Kenya kwa Mbio za Nyika za Dunia. Nataka kuona mwili wangu utakavyoitikia baada ya kushiriki Riadha za Dunia jijini Tokyo,” alisema Kipkorir, akiongeza kuwa wana muda mfupi wa kupumzika kabla ya maandalizi makali kuanza.
Timu ya Kipkorir iliyokuwa na Virginia Nyambura, Kyumbe Munguti na Purity Chepkirui ilitetea taji la mbio za mseto katika Mbio za Nyika za Dunia mwaka 2024 jijini Belgrade, Serbia.
Kenya imeshinda jumla ya mashindano matatu ya mbio za mseto tangu yalipoanzishwa katika makala ya 2017 jijini Kampala, Uganda. Kenya ilitawala makala ya kwanza Kampala, ikapoteza kwa Ethiopia mwaka 2019 mjini Aarhus, Denmark, kabla ya kushinda tena mwaka 2023 Bathurst, Australia na 2024 Belgrade, Serbia.
“AK Nairobi daima imekuwa ikizalisha mabingwa wa dunia, na Kipkorir ni miongoni mwao. Tunataka idadi kubwa ya wanariadha wa Nairobi kuingia katika Timu ya Kenya kuelekea mashindano ya Florida, hasa katika vitengo vya chipukizi,” alisema Mwenyekiti wa AK Nairobi, Barnaba Korir.
Katika upande wa wanawake wa chini ya miaka 20, Cynthia Chepkurui, bingwa wa Afrika wa 3,000m mwaka 2025, ambaye pia ni mshindi wa Sirikwa Classic Cross Country 2024 na Chepsaita Cross Country kilomita sita, anatarajiwa kuwa tishio.
Chepkurui atashindana na Anatasha Cheptoo, bingwa wa Afrika wa 3,000m kuruka viunzi na maji mwaka 2025, na Mercy Chepng’eno Mageso, mshindi wa medali ya shaba katika 2,000m kuruka viunzi na maji wa Afrika U-18.
Mashindano hayo pia yatakuwa sehemu ya Roysambu United Mazingira Day Cross Country ambapo miti 5,000 itapandwa Kasarani kuadhimisha Siku ya Mazingira inayosherehekewa Oktoba 10.
Roysambu United, shirika la kijamii linaloongozwa na wanawake lenye makao yake Kasarani, litatumia mashindano hayo kuhamasisha kuhusu uhifadhi wa mazingira na elimu, kwa mujibu wa maafisa wa shirika hilo.
Faith Mwaura, ambaye ni mwenyekiti wa Roysambu United, alisema kuwa mbali na upanzi miti, tukio hilo pia litakusanya fedha za elimu kwa wanafunzi wanaohitaji msaada.
“Lengo la mashindano haya ya Mbio za Nyika ni kukusanya fedha kwa ajili ya nguzo zetu kuu na kuchangia kwa njia chanya jamii yetu kupitia shughuli mbalimbali za kila mwezi zinazolenga vijana wa eneo la Roysambu, vikundi vya wanawake, na shule za umma,” alisema Mwaura ambaye pia ni mkurugenzi wa Shirika la Maendeleo la Kenya (KDC). – Imetafsiriwa na Geoffrey Anene