Michezo

Ripoti Guikan hapatani na kocha ni porojo – Gor

January 10th, 2019 Kusoma ni dakika: 1

NA CECIL ODONGO

USIMAMIZI wa miamba wa soka nchini Gor Mahia umekanusha vikali madai kwamba mshambulizi Ephrem Guikan hapatani na kocha mpya Hassan Oktay wakisema mwanasoka huyo ni ‘wao’ na kuwa ripoti hizo ni porojo.

Guikan mnamo Jumatano Januari 9, 2019 alionekana akifokafoka na kujizungumzia kama mwehu alipokuwa akiondoka katika uwanja wa MISC Kasarani baada ya kugundua kwamba jina lake lilikosa kwa orodha ya wachezaji 18 walioilemea Posta Rangers 2-1.

Kulingana na Afisa Mkuu Mtendaji wa Gor Mahia Omondi Aduda, Guikan na Oktay wana uhusiano mzuri na tukio la Jumatano lilifasiriwa vibaya na vyombo vya habari na maadui wao ligini.

“Ni kocha huamua mchezaji anayefaa kucheza, wa kuwekwa benchi na wa kutojumuishwa kabisa kwenye orodha ya wachezaji siku ya mechi. Binafsi nimezungumza na Guikana na hakuna la mno kati yake na mkufunzi wa timu,” akasema Aduda akishiriki mahojiano na TaifaLeo.

Aidha afisa huyo wa ngazi ya juu klabuni humo alifichua kwamba uongozi wa Gor Mahia Alhamisi Januari 10 ulimtuma straika huyo kuwakilisha klabu wakati wa kutolewa kwa tuzo za wachezaji za Soya mjini Mombasa.

Raia huyo wa Ivory Coast nusra aihame K’Ogalo Disemba 2018 kabla ya kughairi nia baada ya kocha wa zamani Dylan Kerr ambaye hawakuwa wakipikika na kuiva kwenye kijungu kimoja kuhamia Afrika Kusini.

Nafasi ya kusakata soka hata hivyo imeendelea kudidimia kwa Guikan chini ya kocha wa sasa Hassan Oktay baada ya mabingwa hao mara 17 kumsajili nyota wa zamani wa Harambee Stars Dennis ‘The Menace’ Oliech.

Oliech ndiye alifunga bao la ushindi katika mechi dhidi ya Posta Rangers.

Safu hiyo ya ushambulizi hata hivyo inaendelea kuwaniwa kama mpira wa kona na washambulizi Jacques Tuyisenge kutoka Burundi, Mrwanda Francis Mustapha, Boniface Omondi na Mganda Erisa Ssekisambu.