Ronaldo acheka na nyavu za Cagliari mara mbili na kupaisha Juventus hadi nafasi ya pili Serie A
Na MASHIRIKA
CRISTIANO Ronaldo alifunga mabao mawili katika kipindi cha dakika nne na kuwaongoza mabingwa watetezi wa Ligi Kuu ya Italia (Serie A), Juventus kuwapepeta Cagliari 2-0 mnamo Novemba 21, 2020.
Ushindi huo uliosajiliwa na vijana wa kocha Andrea Pirlo uliwapaisha hadi nafasi ya pili kwenye msimamo wa jedwali la Serie A kwa alama 16, moja nyuma ya viongozi AC Milan ambao wana mchuano mmoja zaidi wa kusakata ili kufikia idadi ya mechi ambazo zimepigwa na Juventus.
Milan walitarajiwa kuchuana na nambari nne Napoli mnamo Novemba 22, 2020 usiku.
Mabao yaliyofungwa na Ronaldo sasa yanamweka Mreno huyo pamoja na Zlatan Ibrahimovic wa AC Milan kileleni mwa orodha ya wafungaji bora wa Serie A hadi kufikia sasa muhula huu.
Juventus kwa sasa wametandaza jumla ya mechi nane, moja zaidi kuliko wapinzani wao wote ambao kwa sasa wamo ndani ya mduara wa tano-bora.
Wakijivunia kusajili ushindi katika mechi nne na kuambulia sare nne, Juventus kwa sasa hawajapoteza mchuano wowote hadi kufikia sasa msimu huu sawa na Milan na Sassuolo wanaoshikilia nafasi ya tatu kwa alama 15, moja zaidi kuliko Napoli.
Juventus waliwahi kupokezwa alama tatu za bwerere na ushindi wa 3-0 mnamo Oktoba 2020 baada ya Napoli waliokuwa wawe wageni wao kukosa kufikia uwanjani kwa hofu ya maambukizi ya virusi vya corona.
MATOKEO YA SERIE A (Novemba 21, 2020):
Juventus 2-0 Cagliari
Crotone 0-2 Lazio
Spezia 0-0 Atalanta