Ronaldo apoteza penalti katika mechi ya Serie A kati ya Juventus na Atalanta
Na MASHIRIKA
CRISTIANO Ronaldo alipoteza penalti katika mchuano wa Ligi Kuu ya Italia (Serie A) ulioshuhudia Juventus wakiambulia sare ya 1-1 dhidi ya Atalanta mnamo Jumatano.
Ilikuwa mara ya sita kwa Juventus kusajili sare kutokana na mechi 12 za hadi kufikia sasa msimu huu wa 2020-21.
Federico Chiesa aliwaweka Juventus ambao ni mabingwa watetezi wa Serie A uongozini katika dakika ya 29. Hilo lilikuwa bao lake la kwanza la Serie A akivalia jezi za Juventus.
Remo Freuler alisawazishia Atalanta katika dakika ya 57.
Ronaldo alipata fursa ya kufungia Juventus bao la ushindi katika dakika ya 68 kupitia penalti baada ya Chiesa kuchezewa visivyo. Hata hivyo, mkwaju wake ulinyakwa na kipa Pierluigi Gollini.
Gollini ambaye pia amewahi kuwadakia Aston Villa, alifanya kazi ya ziada na kumnyima pia Alvaro Morata nafasi kadhaa za wazi.
Licha ya sare sita, Juventus waliendeleza rekodi nzuri ya kutoshindwa katika mechi 12 za hadi kufikia sasa chini ya mkufunzi Andrea Pirlo.
Miamba hao kwa sasa wanashikilia nafasi ya tatu jedwalini kwa alama 24, nne nyuma ya viongozi AC Milan.
Milan kwa upande wao walilazimika kusubiri hadi dakika ya 83 kusawazishiwa na Pierre Kalulu katika sare ya 2-2 waliyolazimishiwa na Genoa. Matokeo hayo pia yaliendeleza rekodi nzuri ya kutoshindwa kwa Milan ligini hadi kufikia sasa msimu huu.
Mattia Destro aliwaweka Genoa uongozini baada ya Davide Calabria kusawazisha.
Kwingineko, Romelu Lukaku alifunga penalti katika kipindi cha pili na kusaidia Inter Milan kusajili ushindi wa 1-0 dhidi ya Napoli waliomshuhudia kiungo Lorenzo Insigne akionyeshwa kadi nyekundu.
Lukaku, Ronaldo na Zlatan Ibrahimovic wa AC Milan sasa wanaongoza orodha ya wafungaji bora wa Serie A kila mmoja akijivunia mabao 10.