• Nairobi
  • Last Updated May 2nd, 2024 8:55 PM
Ronaldo atambisha Juventus katika mechi ya kwanza ya kocha Pirlo kwenye Serie A

Ronaldo atambisha Juventus katika mechi ya kwanza ya kocha Pirlo kwenye Serie A

Na MASHIRIKA

CRISTIANO Ronaldo alifunga bao na kusaidia Juventus inayonolewa na kocha mpya Andrea Pirlo kupepeta Sampdoria ya kocha Claudio Ranieri 3-0 katika Ligi Kuu ya Italia (Serie A).

Kiungo mshambuliaji raia wa Uswidi, Dejan Kulusevski aliwafungulia Juventus ukurasa wa mabao katika dakika ya 13 kabla ya Leonardo Bonucci kufunga la pili katika dakika ya 78.

Ronaldo alizamisha kabisa chombo cha wenyeji wao mwishoni mwa kipindi cha pili na kuhakikisha kwamba Juventus wanaanza vyema kampeni za kutwaa taji la 10 mfululizo kwenye soka ya Serie A.

Bao la Ronaldo ambaye awali alikuwa ameshuhudia makombora yake mawili yakigongwa mwamba wa goli la Sampdoria, lilikuwa zao la ushirikiano mkubwa kati yake na kiungo wa zamani wa Arsenal, Aaron Ramsey.

Mechi hiyo ilihudhuriwa na takriban mashabiki 1,000 jijini Turin.

Hadi alipoteuliwa kuwa kocha wa Juventus mwanzoni mwa Agosti 2020, Pirlo hakuwa na tajriba yoyote ya ukufunzi kambini mwa kikosi cha haiba kubwa.

Kuteuliwa kwake kulichochewa na haja ya kujaza pengo la Maurizio Sarri aliyetimuliwa baada ya Juventus kubanduliwa mapema kwenye soka ya Klabu Bingwa Ulaya (Uefa).

You can share this post!

Mane aongoza Liverpool kupepeta Chelsea ugani Stamford...

Ruto ahimiza wanasiasa wenzake wafikirie jinsi ya kuwatoa...