Michezo

Ruto apongeza Harambee Starlets kupiga Gambia, asema atatimiza ahadi ya Sh5m

Na GEOFFREY ANENE October 24th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

RAIS William Ruto ameahidi kutimiza ahadi yake kwa timu ya taifa ya soka ya wanawake ya watu wazima ya Harambee Starlets ya Sh5 milioni iwapo watazaba Gambia katika mchuano wa mkondo wa kwanza wa kufuzu Kombe la Afrika (WAFCON) 2026 unaosakatwa ugani Nyayo mnamo Oktoba 24, 2025.

Starlets ya kocha Beldine Odemba imepepeta Gambia 3-1 kupitia mabao ya Mwanahalima Adam, Fasila Adhiambo na Shalyne Opiso. Fatoumata Kanteh alitangulia kuweka Gambia kifua mbele dakika ya pili kabla ya Kenya kujibu na mabao matatu.

“Hongera za dhati kwa wachezaji wetu mashujaa wa Harambee Starlets kwa ushindi wa 3-1 dhidi ya Gambia, ushindi thabiti unaoisogeza Kenya karibu zaidi na kufuzu kushiriki WAFCON 2026 nchini Morocco. Ushindi huu ni ushuhuda wa nidhamu, kipaji, na azimio la wachezaji wetu wa soka ya wanawake, pamoja na uongozi imara wa benchi la kiufundi,” akaandika kwenye mtandao wa jamii baada ya mechi hiyo ya mkondo wa kwanza.

Aliongeza, “Mmetutia fahari taifa la Kenya na kuthibitisha nguvu na ukuaji wa michezo ya wanawake nchini. Kadiri mnavyojiandaa kwa mchuano wa marudiano, mjue kuwa taifa zima lipo nyuma yenu. Mafanikio yenu ni fahari yetu. Endeleeni kung’aa, kuleta ushindi, na kuendeleza roho ya Harambee inayotuweka pamoja na kusukuma taifa letu mbele. Hongera Starlets! Kama nilivyoahidi, nitacheza kama mimi!”

Bw. Ruto alikuwa ametoa ahadi hiyo kabla tu ya mechi baada ya kutoa zawadi nyingine ya Sh5m kuwapa vipusa hao motisha. Alikuwa amewaahidi Sh2.5m endapo wangetoka sare.

Kwa mechi ya marudiano nchini Senegal hapo Oktoba 27, Rais ameahidi kuongeza motisha ya Sh1m kwa kila mchezaji iwapo Starlets itashinda na kufuzu kushiriki WAFCON2026, na Sh500,000 kwa kila mchezaji endapo watatoka sare na bado kufuzu.

Mshindi kati ya Harambee Starlets na Gambia baada ya mikondo miwili ataingia WAFCON2026 itakayohusisha mataifa 16 kutoka 12 yaliyoshiriki makala ya 2024.

Kenya ilishiriki WAFCON mara ya kwanza kabisa na mwisho mwaka 2016 nchini Cameroon. Inapigania kurejea katika mashindano hayo ha haiba baada ya kukosa makala matatu mfululizo (2028, 2022 na 2024).

Motisha hizo zinathibitisha kwa mara nyingine dira thabiti ya Bw. Ruto ya kuhamasisha, kutuza, na kibiashara kukuza vipaji vya michezo vya Wakenya, kubadilisha vipaji na hamasa kuwa fursa, na kuiweka Kenya katika nafasi ya kuwa nguvu ya kutisha katika soka ya Afrika na michezo ya kimataifa.