Michezo

Ruto, Raila waongoza Wakenya kumpongeza Kipyegon kwa kuvunja rekodi tena


MALKIA wa mbio za mita 1,500 za dunia na Olimpiki, Faith Kipyegon anaendelea kumiminiwa sifa baada ya kuvunja rekodi yake ya dunia katika umbali huo kwenye duru ya nane ya Diamond League jijini Paris, Ufaransa, Jumapili.

Kipyegon ameshinda taji kwa dakika 3:49.04, akifuta rekodi ya 3:49.11 aliyoweka mjini Florence nchini Italia mwaka jana.

Mtimkaji huyo mwenye umri wa miaka 30 anasalia mwanamke wa kwanza kukamilisha 1,500m chini ya 3:50.00.

“Faith Kipyegon kwa mara nyingine ameandikisha historia. Pongezi kwa kuvunja rekodi yako ya dunia. Ushindi wako ni ushuhuda tosha wa matunda ya kufanya bidii na kujituma, funzo muhimu linalofaa kuwapa wanamichezo chipukizi motisha wanaokuenzi,” akasema Rais William Ruto.

Kinara wa Azimio Raila Odinga akasema, “Faith Kipyegon, kazi yako safi ya kufuta rekodi yako ya dunia jijini Paris inatia moyo sana. Kujitolea kwako na mapenzi yako yanafanya wanamichezo wa Kenya wapate kujiamini. Endelea kufanya kazi unayopenda ya kukimbia na kung’aa!”

“Matokeo ya kufana kutoka kwa Faith Kipyegon kuvunja rekodi yake ya dunia ya 1,500m kwenye riadha za Paris Diamond League. Pongezi kwa kuendelea kupatia kizazi kijacho motisha ya kutafuta mafanikio na kutimiza ndoto zao. Kenya inajivunja kazi yako,” akasema waziri wa zamani Charles Keter.

Kipyegon alifuatwa kwa karibu na Jessica Hull kutoka Australia (3:50.83), Muingereza Laura Muir (3:53.79), Linden Hall kutoka Australia (3:56.40), Muingereza Georgia Bell (3:56.54) na Mkenya Susan Ejore (3:57.26), mtawalia.

“Nilijua inawezekana kupata rekodi ya dunia kwa sababu nilikimbia kasi ya juu nchini Kenya,” akasema Kipyegon baada ya ushindi wake mpya.

“Nilikuwa nakuja hapa kukimbia mbio zangu kama kawaida na kuona hali yangu ya kimwili ilivyo nikilenga kuhifadhi taji langu la Olimpiki jijini Paris,” akaongeza katika siku ambayo ni Wakenya wachache walifanya vyema kwenye Paris Diamond League.

Jacob Krop alitawala 3,000m kwa dakika 7:28.83 naye mshikilizi wa rekodi ya dunia mbio za 3,000m kuruka viunzi na maji Beatrice Chepkoech akasikitisha katika nafasi ya tisa.

Emmanuel Wanyonyi aliyejivunia muda bora mwaka huu baada ya kukamilisha 800m kwa dakika 1:41.70 ugani Nyayo jijini Nairobi mnamo Juni 15 akifuzu Olimpiki, aliridhika na nafasi ya pili kwa muda wake mpya bora wa 1:41.58.

Djamel Sedjati kutoka Algeria alitwaa taji la Paris Diamond League kwa muda mpya bora dunia mwaka huu wa 1:41.56. Sedjati alikosa rekodi ya Paris Diamond League ya Mkenya David Rudisha kwa sekunde 0.02. Alikuwa na muda bora wa 1:43.06.

Mfaransa Gabriel Tual (1:41.61) na Wakenya Aaron Cheminingwa (1:42.08) na bingwa wa zamani wa Jumuiya ya Madola Wyclife Kinyamal (1:42.08) walifunga mduara wa tano-bora kutoka orodha ya washiriki 12.

Mshindi wa medali ya fedha kwenye Michezo ya Afrika Amos Serem na bingwa wa Jumuiya ya Madola Abraham Kibiwott nao waliridhika na nafasi ya pili na tatu kwa dakika 8:02.36 na 8:06.70 katika 3,000m kuruka viunzi na maji. Walimaliza nyuma ya Muethiopia Abrham Sime (8:02.36).

Leonard Bett alikamata nafasi ya nane kwa 8:12.97 nao Lawrence Kipsang, Wilberforce Kones na Simon Kiprop wakashindwa kukamilisha kitengo hicho kilichovutia washiriki 18.

Serem, Koech na Kibiwott wako katika kikosi cha timu ya Olimpiki ya Kenya.

Kuna zawadi za kumaliza ndani ya nafasi nane za kwanza kwenye kila duru ya Diamond League zikiwemo Sh1.2 milioni, Sh763,068 na Sh445,123 kwa watimkaji watatu wa kwanza, mtawalia.