Sajili mpya wa Barcelona Miralem Pjanic augua Covid-19
Na CHRIS ADUNGO
KIUNGO matata wa Barcelona, Miralem Pjanic amepatikana na virusi vya corona.
Hadi alipofanyiwa vipimo vya afya, nyota huyo mzawa wa Bosnia, 30, hakuwa akionyesha dalili zozote za kuugua ugonjwa wa Covid-19.
Kwa sasa amejitenga nyumbani kwake na anatarajiwa kusafiri hadi kambini mwa Barcelona baada ya kipindi cha siku 15.
Pjanic aliingia katika sajili rasmi ya Barcelona mwishoni mwa msimu huu katika makubaliano yaliyoshuhudia waajiri wake wa zamani, Juventus wakimtwaa kiungo Arthur Melo kutoka uwanjani Camp Nou.
Barcelona wamepania kujisuka upya kwa minajili ya kampeni za msimu ujao baada ya kuambulia nafasi ya pili kwenye Ligi Kuu ya Uhispania (La Liga) msimu huu, kuondolewa mapema kwenye Copa del Rey na kudhalilishwa 8-2 na Bayern Munich kwenye robo-fainali za Klabu Bingwa Ulaya (UEFA).
Matokeo duni yaliyoshuhudia Barcelona wakikamilisha kampeni za msimu huu bila taji lolote kwa mara ya kwanza tangu 2007-08, yalichangia kutimuliwa kwa kocha Quique Setien na nafasi yake kuchukuliwa na Ronald Koeman aliyeagana na timu ya taifa ya Uholanzi.
Msimu mpya wa kivumbi cha La Liga umeratibiwa kuanza Septemba 12, 2020.