Sajili mpya wa Tusker alenga kuitwa Harambee Stars
Na CECIL ODONGO
KIFAA kipya cha Tusker FC Faraj Ominde ameahidi kudhihirisha ukwasi wake wa talanta klabuni na kuvutia macho ya benchi ya kiufundi ya timu ya taifa Harambee Stars.
Kiungo huyo aliyetoroka njaa kutoka kwa Chemeli FC alimwaga wino kwa kandarasi ya miaka mitatu itakayohakikisha ananoga kampeni za waunda mvinyo hao hadi mwaka wa 2021.
Mwanadimba huyo anatarajiwa kuwania nafasi yake katika safu ya kati ya Tusker inayojivunia baadhi ya mastaa bora katika ligi ya KPL.
Hata hivyo amesisitiza kwamba analenga kujiimarisha na kutimiza ndoto yake ya kuitwa katika kikosi cha timu ya taifa huku akitumai kwamba milango ya heri itamfungulia na apate ujira katika klabu za ughaibuni.
‘’Nafurahi sana kutimiza ndoto yangu ya kujiunga na timu hii. Nalenga kuimarisha safu ya kati ambayo tayari ni dhabiti na nimeshiriki mazoezi nao kwa wiki moja. Ninahisi nimekaribishwa vyema sana,” akasema Ominde baada ya kutia saini mkataba huo.
Mchezaji huyo ni sajili wa pili kwa Tusker baada ya kusainiwa kwa mshambulizi David Juma kutoka Bidco United.
Kocha wa Tusker aliyechukua usukani kutoka kwa mganda Sam Ssimbwa analenga kukiimarisha kikosi hicho ambacho kilisuasua na kusajili matokeo yasiyoridhisha katika mkondo wa kwanza wa ligi.
Mabingwa hao mara 11 wanashikilia nafasi ya 11 kwenye msimamo wa jedwali la ligi ya KPL kwa alama 23 huku wakionekana kusalimu amri ya kutwaa ubingwa wa mwaka huu. Mwanya wa alama 14 inawatenganisha na viongozi wa ligi Gor Mahia.
Tusker wanatarajiwa kusakata mechi yao ya 20 wikendi hii dhidi ya Posta Rangers katika uwanja wao wa nyumbani wa Ruaraka mjini Nairobi.