• Nairobi
  • Last Updated April 30th, 2024 8:19 PM
Saka, Lacazette wasaidia Arsenal kupepeta Wolves ligini

Saka, Lacazette wasaidia Arsenal kupepeta Wolves ligini

Na CHRIS ADUNGO

BUKAYO Saka alisherehekea kupokezwa kwake mkataba mpya kambini mwa Arsenal kwa kuwafungia miamba hao wa zamani wa soka ya Uingereza bao lililochangia kichapo cha 2-0 dhidi ya Wolves uwanjani Molineux.

Ushindi huo wa Arsenal uliwayumbisha Wolves na kudidimiza matumaini yao ya kumaliza kampeni za Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) miongoni mwa vikosi vinne vya kwanza msimu huu na hivyo kufuzu kwa kipute cha Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) muhula ujao.

Bao la Saka ambaye alisifiwa pakubwa na kocha wake Mikel Arteta kwa kupuuza Liverpool na Borussia Dortmund waliokuwa wakimhemea hadi wiki iliyopita, lilikuwa lake la kwanza katika EPL.

Chipukizi huyo mzawa wa Uingereza aliwaweka Arsenal kifua mbele kunako dakika ya 43 kabla ya fowadi Alexandre Lacazette aliyetokea benchi katika dakika ya 79 kuzamisha kabisa chombo cha Wolves mwishoni mwa kipindi cha pili.

Ushindi wa Arsenal ulikuwa wao wa nne mfululizo tangu kurejelewa kwa soka ya Uingereza iliyokuwa imesitishwa kwa muda kwa sababu ya janga la corona.

Wolves walijibwaga uwanjani kwa minajili ya mchuano huo wakitawaliwa na hamasa ya kusajili ushindi ili kuepuka presha kutoka kwa Leicester City na Manchester United walioibuka washindi wa mechi zao za awali na kuweka hai matumaini ya kutinga nne-bora muhula huu.

Chini ya kocha Nuno Espirito Santo, Wolves walisalia kujutia utepetevu wa washambuliaji wao walioshindwa kutumia nafasi tatu za wazi walizozipata kupitia kwa Diogo Jota na Adama Traore katika kipindi cha pili.

Wolves kwa sasa wanashikilia nafasi ya sita jedwalini kwa alama 52, tatu pekee mbele ya Arsenal ambao pia wanafukuzia fursa ya kushiriki soka ya bara Ulaya msimu ujao na ubingwa wa Kombe la FA muhula huu.

Tangu kupigwa na Manchester City na chombo chao kuzamishwa na Brighton, Arsenal wamepania kujinyanyua na wamesajili ushindi dhidi ya Southampton, Norwich na Wolves huku wakijikatia pia tiketi ya kuvaana na Manchester City kwenye nusu-fainali ya Kombe la FA baada ya kuwabandua Sheffield United kwenye hatua ya nane-bora.

Wolves walishuka dimbani kwa gozi dhidi ya Arsenal wakiwa na hamasa tele kutokana na ushindi dhidi ya West Ham United, Bournemouth na Aston Villa. Bao la Saka lilikuwa la kwanza kwa Wolves kufungwa katika kipindi cha zaidi ya dakika 450 uwanjani tangu kurejelewa kwa kivumbi cha EPL.

You can share this post!

Ronaldo afunga frikiki na kuweka rekodi ya utitigaji nyavu...

Bayern Munich wapepeta Bayer Leverkusen 4-2 kujizolea taji...

adminleo