Salah ahifadhi taji la mwanasoka bora Afrika
Na GEOFFREY ANENE
STRAIKA wa Liverpool na Misri Mohamed Salah ametangazwa mshindi wa Mwanasoka Bora wa Bara Afrika mwaka 2018 Januari 8, 2019 usiku na Shirikisho la Soka barani Afrika (CAF) jijini Dakar nchini Senegal.
Salah alipigiwa upatu mkubwa kutetea taji lake. Aling’ara sana katika klabu yake ya Liverpool msimu 2017-2018 na kunyaua taji hilo baada ya kuibuka mfungaji bora katika Ligi Kuu ya Uingereza.
Ingawa alianza msimu 2018-2019 vibaya, amepata makali yake na kumweka pazuri kushinda taji hili la kifahari kwa mara ya pili mfululizo.
Alikuwa na mchango mkubwa katika timu yake ya taifa kufuzu kushiriki Kombe la Afrika (AFCON) mwaka 2019, ambalo mwenyeji atafahamika Januari 9 kati ya Misri na Afrika Kusini baada ya Cameroon kupokonywa majukumu hayo kwa kutokuwa tayari.
Salah, 26, anawania taji la mwanasoka bora wa Afrika dhidi ya mshambuliaji mwenza kutoka klabu ya Liverpool, Sadio Mane, na mvamizi wa klabu ya Arsenal, Pierre-Emerick Aubameyang.
Mgabon Aubameyang amefika fainali tano za wachezaji watatu wa mwisho tangu mwaka 2014. Mwaka 2014, Aubameyang alimaliza katika nafasi ya pili nyuma ya kiungo mbunifu wa Ivory Coast, Yaya Toure.
Alimpiku Toure na kuibuka bingwa mwaka 2015 kabla ya kumaliza wa pili nyuma ya Riyad Mahrez mwaka uliofuata, ambao ulishuhudia Mane akishikilia nafasi ya tatu. Mara hiyo yote nne alikuwa mchezaji wa Borussia Dortmund nchini Uingereza.
Akiwa mchezaji wa Arsenal, Aubameyang alimaliza katika nafasi ya tatu mwaka 2017 nyuma ya mshindi na mvamizi matata Mohamed Salah kutoka Misri na mshambuliaji Mane. Aubameyang, Salah na Mane wamefungia klabu zao mabao 14, 13 na manane ligini msimu huu, mtawalia.
Hafla yenyewe ya kutuza mwanasoka wa mwaka 2018 itaandaliwa katika jumba la mikutano la Abdou Diouf. Kulingana na CAF, wageni 1,250 wanatarajiwa kuhudhuria wakiwemo Marais Macky Sall (Senegal) na George Weah (Liberia) na Rais wa Shirikisho la Soka duniani (FIFA) Gianni Infantino na mwenzake kutoka CAF, Ahmad Ahmad. Mbali na mwanasoka bora mwanamume kutawazwa, CAF pia itatangaza washindi wa vitengo vya mwanasoka bora mwanamke, kocha bora wa mwaka, timu bora ya taifa na kadhalika.
Mwanasoka bora wa mwaka (mwanamume):
Mshindi Mwaka Taifa
Mohamed Salah 2017 Misri
Riyad Mahrez 2016 Algeria
Pierre-Emerick Aubameyang 2015 Gabon
Yaya Toure 2014 Ivory Coast
Yaya Toure 2013 Ivory Coast
Yaya Toure 2012 Ivory Coast
Yaya Toure 2011 Ivory Coast
Samuel Eto’o 2010 Cameroon
Didier Drogba 2009 Ivory Coast
Emmanuel Adebayor 2008 Togo
Frederic Kanoute 2007 Mali
Didier Drogba 2006 Ivory Coast
Samuel Eto’oo 2005 Cameroon
Samuel Eto’oo 2004 Cameroon
Samuel Eto’oo 2003 Cameroon
El Hadji Diouf 2002 Senegal
El Hadji Diouf 2001 Senegal
Patrick M’Boma 2000 Cameroon
Nwankwo Kanu 1999 Nigeria
Mustapha Hadji 1998 Morocco
Victor Ikpeba 1997 Nigeria
Nwankwo Kanu 1996 Nigeria
George Weah 1995 Liberia
Emmanuel Amunike 1994 Nigeria
Rashidi Yekini 1993 Nigeria
Abedi Pele 1992 Ghana