Salah avunja rekodi ya ufungaji wa Liverpool kwenye kipute cha UEFA
Na MASHIRIKA
KOCHA Jurgen Klopp wa Liverpool amesema kwamba nyota Mohamed Salah ana idadi kubwa ya mabao yanayotosha kumsadikisha yeyote kuwa mshambuliaji huyo raia wa Misri ni miongoni mwa wanasoka bora zaidi duniani kwa sasa.
Bao lililofungwa na Salah katika sare ya 1-1 dhidi ya Midtjylland ya Denmark katika mechi ya Kundi D ya Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) mnamo Disemba 9, 2020, lilimwezesha Salah kuweka rekodi ya kuwa mfungaji bora wa muda wote wa Liverpool katika soka hiyo ya bara Ulaya.
Liverpool walishuka dimbani wakiwa tayari wamefuzu kwa hatua ya 16-bora baada ya mwanzo mzuri kwenye kampeni za makundi kuwapa uhakika wa kumaliza kileleni.
Hata hivyo, bado walitawaliwa na kiu ya kufunga mabao dhidi ya wenyeji wao Midtjylland huku Salah akiwaweka waajiri wake uongozini baada ya sekunde 55 pekee za kipindi cha kwanza.
Bao hilo ndilo la haraka zaidi kwa Liverpool kuwahi kufunga katika kivumbi cha UEFA na lilimwezesha Salah kufikisha jumla ya magoli 22 kapuni mwake kutokana na kipute hicho. Ufanisi huo ulimshuhudia fowadi huyo wa zamani wa Chelsea na AS Roma akiipiku rekodi ya aliyekuwa kiungo matata wa Liverpool, Steven Gerrard.
“Salah ni mchezaji wa haiba kubwa anayejivunia utajiri wa kipaji. Ana ushawishi mkubwa uwanjani na ni tishio kubwa kwa wapinzani kila anapokuwa na mpira,” akasema Klopp.
Mbali na Salah, wachezaji wengine walioridhisha zaidi kambini mwa Liverpool ni Diogo Jota na Divock Origi waliomtatiza pakubwa kipa Jesper Hansen wa Midtjylland.
Kichapo cha 2-0 ambacho Liverpool walipokezwa na Atalanta ya Italia mnamo Novemba 25, 2020, ndicho cha pekee kwa masogora wa Klopp ambao ni mabingwa mara sita wa soka ya bara Ulaya, kupokezwa kwenye kampeni za UEFA msimu huu.
Kwa waliingia uwanjani wakijivunia tayari kufuzu kwa hatua ya mwondoano, Liverpool waliwajibisha kikosi kichanga zaidi kilichokuwa chini ya unahodha wa beki Trent Alexander-Arnold.
Kikosi hicho kilichocheza dhidi ya Midtjylland, kilijivunia pia maarifa ya chipukizi Rhys Williams, Leighton Clarkson na Billy Koumetio.