Sare yaletea Liverpool mchecheto ligi ikipamba moto
NA AFP
MERSEYSIDE
Liverpool, Uingereza
HUKU zikisalia mechi 13 kabla ya kumalizika kwa ratiba ya Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) msimu huu, kwa mara nyingine ni hofu kuu kwa mashabiki wa Liverpool.
Hii ni kutokana na sare mbili mfululizo ambazo klabu hiyo imepata katika mechi za karibuni ambazo zimefanya mbio za kutwaa ubingwa wa ligi hiyo kuwa ngumu kubashiri.
Hali hii inawakumbusha mashabiki hao machungu waliyopitia misimu ya 2008-09 na 2013-14 ambapo timu hiyo ilikosa kutwaa ubingwa dakika ya mwisho.
Swali miongoni mwa mashabiki wa soka ni, je, mkosi huu unaweza kuandama Liverpool kwa mara ya tatu?
Liverpool maarufu kama Majogoo wa Jiji au The Reds haijatwaa ubingwa wa EPL tangu 1990, na juzi ilikuwa na nafasi nzuri ya kutanua pengo la uongozi kileleni kwa alama kubwa, hali ambayo ingeipa nafasi nzuri ya kushinda taji hilo.
Walipokutana na Manchester City mnamo Januari 3, walikuwa na uwezekano wa kutanua pengo kwa alama 10, kwani walikuwa wakiongoza kwa alama saba kabla ya mechi hiyo, lakini wakaipoteza mechi hiyo kwa 2-1 na kufanya pengo lifikie pointi nne.
Wakati Manchester City walipofungwa 2-1 na Newcastle United pia wangerejea pazuri kupanua pengo hadi alama saba, iwapo wangeifunga Leicester City, siku moja baadaye, lakini wakatoka sare 1-1 katika mechi hiyo iliyochezwa Januari 30, na kufanya pengo kuwa tano.
Siku hiyo, kocha Jurgen Klopp alidai theluji iliyokuwa imejaa uwanjani ndio iliyowazuia kufunga mabao.
Jumatatu usiku, Liverpool ilirejea uwanjani usiku dhidi ya West Ham United lakini ikatoka sare 1-1, baada ya Manchester kuwanyuka Arsenal 2-1 mwishoni mwa wiki, matokeo ambayo yamepunguza pengo kuwa pointi tatu pekee baina yao!
Huku ni kuteleza pakubwa kwa Liverpool, lakini habari njema kwa Manchester City ambazo tofauti kati yao ilikuwa pointi tisa kufikia Desemba 29.
Endapo Manchester itaichapa Everton leo usiku, itachukuwa uongozi wa msimamo wa ligi hii kwa tofauti ya mabao.
Tottenham ambao wana pointi 57 pia wangalipo kwenye kinyang’anyiro hicho cha kuwania ubingwa, kwani wako alama tano pekee nyuma ya Liverpool.
Historia haipo upande wa Liverpool katika kampeni hii ya kuwania ubingwa wa EPL, kwani limekuwa jambo la kawaida kwa klabu hiyo hata baada ya kuongoza wakati wa Siku Kuu ya Krismasi na Mwaka Mpya.
Katika misimu 10 iliyopita, ubingwa wa EPL ulienda kwa klabu inayokuwa uongozini wakati wa msimu wa Siku Kuu ya Krismasi na Mwaka Mpya kutwaa ubingwa.
Ni mara mbili pekee ambazo haikuwa hivyo, msimu wa 2008-09 na 2013-14 wakati ambapo Liverpool ilikuwa uongozini.