Serikali yaahidi kuwasaidia Chipu kwa kuibuka mabingwa wa Afrika raga U-20
Na GEOFFREY ANENE
Serikali imeahidi kusaidia timu ya chipukizi ya Kenya kushiriki Raga ya Dunia ya wachezaji wasiozidi umri wa miaka 20 ya daraja ya pili baada ya timu hiyo almaarufu Chipu kuchabanga Namibia kwa alama 21-18 katika fainali ya Bara Afrika jijini Nairobi, Jumapili.
“Tutasaidia Chipu asilimia 100 katika maandalizi yake na safari yake ya Brazil kwa michuano ya dunia,” amesema Katibu katika Wizara ya Michezo, Kirimi Kaberia na kuongeza kwamba alifurahishwa na bidii na mchezo wa Chipu hasa baada ya kupata tiketi zaidi ya miaka 10 tangu Kenya iandae Raga ya Dunia jijini Nairobi mwaka 2009.
Kenya inaungana na wenyeji wa mashindano ya dunia Brazil pamoja na Hong Kong (Asia), Uruguay (Amerika Kusini), Ureno (Ulaya), Tonga (Oceania) na Japan iliyotemwa kutoka mashindano ya dunia ya daraja ya juu.
Ilizamisha chombo cha Namibia kupitia miguso ya Brian Amaitsa, Beldad Oget, nahodha Bonface Ochieng’ na penalti ya Andrew Matoka aliyeibuka mchezaji bora wa mechi hiyo kali.
Chipu ya kocha Paul Odera haikupata ushindi kwa urahisi. Ilihitaji kutoka chini mara mbili na kupata ushindi huo wa kihistoria.
Wakati mmoja wa mechi Kenya ilikuwa watu 13 dhidi ya Wanamibia 15 baada ya Emanuel Silungi na Samuel Were kuonyeshwa kadi ya njano na kukaa nje dakika tano. Matoka aligonga msumari wa mwisho kupitia penalti safi dakika ya 77.
Kenya sasa itaelekea nchini Brazil mnamo Julai 9-21 mwaka 2019 kuwania tiketi ya kupandishwa katika daraja ya kwanza ya dunia.
Fainali ilitanguliwa na mechi ya kutafuta nambari tatu ambayo Senegal ilibwaga Tunisia 28-16 na kujihakikishia mwaka mwingine katika mashindano ya daraja ya juu ya Afrika. Tunisia itashiriki mashindano ya Afrika ya daraja ya pili mwaka 2020.