Michezo

Sh10 milioni pap! Jumapili ya kismati Sawe akiwika marathon yake ya kwanza

Na GEOFFREY ANENE December 2nd, 2024 Kusoma ni dakika: 2

ILIKUWA Jumapili ya baraka tele kwa Sebastian Sawe alipotia mfukoni Sh10.2 milioni kufuatia ushindi wake wa kwanza kabisa wa mbio za marathon jijini Valencia, Uhispania.

Bingwa huyo wa dunia wa mbio za 21km alitangaza kuwasili katika ngazi ya juu ya marathon – kilomita 42- kwa kishindo akitwaa taji la Valencia Marathon katika muda wa saa 2:02:05 Jumapili mchana.

Alifuatwa kwa karibu na Muethiopia Deresa Geleta (2:02:38) na Mkenya mwingine Daniel Mateiko ambaye pia alijitosa katika marathon kwa mara ya kwanza kabisa (2:04:24). Mateiko ni mshindi wa nishani ya fedha mbio za 21km duniani.

Sawe asherehekea na bendera ya Kenya baada ya kushinda mbio hizo nchini Uhispania. PICHA | REUTERS

Mtanzania Alphonce Simbu (2:04:38) na Tadesse Abraham kutoka Uswisi (2:04:40) walikamilisha nafasi tano za kwanza, mtawalia.

Mkenya wa pekee katika kitengo cha wanawake Evaline Chrichir alikamata nafasi ya nne kwa 2:18:35 katika kitengo hicho, nyuma ya Muethiopia Megertu Alemu (2:16:49), Mganda Stella Chesang (2:18:26) na Muethiopia Tiruye Mesfin (2:18:35). Nafasi ya pili hadi tano zilituzwa Sh6.1m, Sh4.1m, Sh2.4m na Sh1.3m, mtawalia.

Nchini Japan, Patrick Mathenge aliridhika na nafasi ya tatu kwenye Fukuoka Marathon kwa 2:08:28, nyuma ya Wajapani Yuya Yoshida (2:05:16) na Yusuke Nishiyama (2:06:54).

Wakenya Titus Kipruto (2:06:30) na Solomon Yego (2:06:34) walimfuata mshindi Samson Amare kutoka Eritrea (2:06:26) katika nafasi tatu za kwanza za Shanghai Marathon.

Rael Cherop naye alitawala Torino City Marathon kwa 2:33:51, akifuatwa na Mwitaliano Catherine Bertone (2:39:01) na Janet Jelagat (2:43:29) naye John Mungai akawa nambari tatu kwa upande wa wanaume (2:17:15).

Christine Njoki ashinda kitengo cha 10km mashindano ya kwanza kabisa ya TechRun-EldoHub, jijini Eldoret mnamo Desemba 01, 2024. PICHA | JARED NYATAYA

Jijini Eldoret, Kenya, Christine Njoki naye alinyakua taji la mbio za 10km za makala ya kwanza ya EldoHub TechRun hapo Jumapili asubuhi.

Njoki alitwaa taji hilo kwa dakika 32 na sekunde 35.3 akifuatiwa na Maurine Toroitich (32:53.3) na Christine Chesiro (33:02.2).

Nao John Lomon (29:19.9), Benard Langat (29:34.4) na Cornelius Kemboi (29:47.9) wakafagia tatu za kwanza katika kitengo cha wanaume, mtawalia.

John Lomon akielekea kushinda 10km makala ya kwanza ya TechRun-EldoHub, jijini Eldoret. PICHA | JARED NYATAYA

Katika jiji kuu Nairobi, mbio za 21km za kuadhimisha miaka 40 tangu kisa cha kwanza cha ukimwi nchini Kenya kiripotiwe ziliandaliwa katika Siku ya Ukimwi Duniani hapo Jumapili.

Waziri wa Afya Dkt Deborah Barasa alisema kuwa muda unaipa Kenya kisogo kuangamiza ukimwi kufikia mwaka 2030. Aliongeza kwamba kuna watu 1.4 milioni nchini Kenya wanaoishi na virusi vya HIV, asilimia 97 wanapata matibabu.