Michezo

Sharks yarejea mazoezini kujiandaa kwa mlima wa KPL

January 29th, 2019 Kusoma ni dakika: 1

Na GEOFFREY ANENE

MABINGWA wapya wa soka ya kimataifa ya SportPesa Super Cup, Kariobangi Sharks wamerejea nchini na kurejelea mazoezi bila karamu ili kujiandalia mechi tatu kali watakazosakata ndani ya siku saba.

Sharks ya kocha William Muluya ilizima Bandari 1-0 kupitia bao safi kutoka kwa Harrison Mwendwa na kushinda makala ya tatu ya SportPesa Super Cup jijini Dar es Salaam, Tanzania mnamo Januari 27, 2019.

Ilijishindia tuzo ya washindi ya Sh3 milioni pamoja na tiketi ya kukutana na Everton kutoka nchini Uingereza katika mechi ya kirafiki baadaye mwaka huu.

Kwa kawaida ufanisi huu pengine ungestahili sherehe. Hata hivyo, Afisa Mkuu Mtendaji wa Kariobangi Sharks Lynda Ambiyo amethibitisha hawataandalia timu karamu yoyote. “Timu inawasili saa kumi na moja na dakika 25 Jumatatu kutoka Tanzania. Tuna mechi zinazokaribiana kwa hivyo hatuna muda kabisa wa kuandaa karamu, bali kurejea kazini,” Ambiyo anasema.

Sharks, ambayo inashikilia nafasi ya tano ligini kwa alama 14 kutokana na mechi nane, itapepetana na viongozi na mabingwa wa mwaka 2008 Mathare United mnamo Januari 30 kabla ya kumenyana na  washindi wa mwaka 2009 Sofapaka hapo Februari 2 na kisha kuvaana na wafalme wa mwaka 2003, 2004, 2005 na 2010 Ulinzi Stars mnamo Februari 6. Mechi hizi tatu zitakuwa katika ardhi ya Sharks.

Vijana wa Muluya pamoja na Mathare na Bandari ndizo klabu pekee hazijapoteza mechi katika ligi hii ya klabu 18. Habari kuhusu mechi kati ya Sharks na Everton bado ni finyu. Tarehe bado haijatangazwa pamoja na uwanja utakaotumika.