Michezo

Shujaa kuanza kampeni za kufuzu kwa Olimpiki Tokyo

October 31st, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na CHRIS ADUNGO

KIKOSI cha Kenya cha wachezaji saba kila upande, Shujaa, kitafungua kampeni za kufuzu kwa Olimpiki za Tokyo 2020 dhidi ya Ivory Coast mnamo Novemba 2019 jijini Johannesburg, Afrika Kusini.

Zimbabwe ambao ni mabingwa wa Africa Sevens, watapimana ubabe na Nigeria huku Uganda wakipangwa kuvaana na Mauritius.

Katika mechi nyinginezo za raundi ya kwanza, Madagascar watamenyana na Botswana, Zambia wachuane na Ghana, Tunisia wakwaruzane na Namibia huku Senegal wakionana na Morocco.

Kwa mujibu wa Shirikisho la Raga la Afrika, mfumo tofauti utatumika katika makala ya mwaka huu ambayo yataleta mataifa 14 tofauti ambayo yameorodheshwa kulingana na matokeo yao ya mwaka uliopita.

Mfumo wa 1 vs 14, 2 vs 13, 3 vs 12, 4 vs 11, 5 vs 10, 6 vs 9, 7 vs 8 ndio utakaotumiwa katika mchujo wa kutafuta wapinzani wa raundi ya pili. Washindi wa kila kundi watafaulu kusonga mbele na kujumuishwa na timu itakayoambulia nafasi ya pili kwa alama za juu zaidi ili kuunga timu ya mataifa manane yatakayopangwa katika makundi mawili ya vikosi vinne kila moja.

Washindi wa mechi ya kwanza, nne na tano wataungana na kikosi kitakachoambulia nafasi ya pili kwa alama nyingi zaidi kuunga Kundi A. Kundi B litajumuisha vikosi vitakavyoibuka na ushindi katika mechi ya pili, tatu, sita na saba. Vikosi vingine sita vitakavyobanduliwa mapema vitapangwa katika makundi ya timu tatu kila moja ili kuwania taji dogo.

Ili kujifua vilivyo kwa kampeni hizo, wanaraga wa Kenya tayari wameingia kambini mwa mazoezi ya siku nne. Wengi wao ni wale waliounga kikosi cha Kenya Morans kilichowazamisha Afrika Kusini 19-14 majuma mawili yaliyopita na kunyakua taji la Safari Sevens.

Kocha wa Shujaa, Paul Feeney anajivunia kikosi cha wachezaji 12 wa haiba kubwa ambao atapania kuwategemea nchini Afrika Kusini na katika kampeni za Raga ya Dunia zitakazoanza rasmi Dubai mnamo Disemba 2019.

“Wachezaji wanazoea mbinu mpya za ukufunzi wangu na dalili zote zinaashiria kwamba watafuzu kwa Olimpiki za mwaka ujao nchini Japan na hata kupiga hatua zaidi katika duru mbalimbali za Raga ya Dunia,” akasema Feeney aliyeteuliwa mwezi jana kujaza nafasi ya Paul Mutunga.

Jeraha la Injera

Pigo kubwa zaidi kwa Shujaa huenda likawa ulazima wa kuzikosa huduma za mwanaraga matata, Collins Injera anayeuguza jeraha.

Injera anayeshikilia rekodi ya kitaifa ya kufungia Kenya idadi kubwa zaidi ya trai katika raga ya dunia anauguza jeraha la mkono alilolipata wakati wa kivumbi cha Safari Sevens yapata wiki mbili zilizopita.

Kipute hicho kilikuwa cha kwanza kwa Injera ambaye ni mwanaraga wa Mwamba RFC kushiriki ndani ya jezi za taifa tangu Juni 2018.

“Anazidi kutibiwa na kwa sasa anaendelea vyema. Ingawa kutokuwapo kwake ni pigo kubwa kwa kikosi, itakuwa ni fursa kwa mchezaji mwingine kudhihirisha ukubwa wa uwezo wake,” akasema Feeney mwishoni mwa kipindi cha mazoezi uwanjani RFUEA, Nairobi.

Hata hivyo, Shujaa wamepigwa jeki zaidi na marejeo ya Billy Odhiambo aliyekosa kushiriki mapambano ya Safari Sevens.