Shujaa mabingwa wapya wa Afrika
Na GEOFFREY ANENE
Timu ya taifa ya raga ya wachezaji saba kila upande ya Kenya almaarufu Shujaa imemaliza ukame wa miaka mitatu bila taji la Kombe la Afrika baada ya kupepeta Uganda 33-0 katika fainali ya Jumamosi jijini Johannesburg nchini Afrika Kusini.
Mbali na kuibuka wafalme wapya wa Bara Afrika, vijana wa kocha Paul Feeney pia wamejikatia tiketi ya kushiriki Olimpiki ya mwaka 2020 moja kwa moja.
Shujaa, ambayo ilifanya vibaya sana raga hii ilipojumuishwa kwenye Olimpiki mwaka 2016 nchini Brazil, ilikuwa inakutana na Uganda kwa mara ya pili jijini Johannesburg.
Ilibwaga majirani hao wake 24-7 katika mechi ya makundi kabla ya kudhirihisha uweledi huo wake katika fainali kupitia miguso ya nahodha Andrew Amonde pamoja Daniel Taabu, Jeff Oluoch na Oscar Dennis aliyefunga miguso miwili.
Kenya, ambayo iliwahi kuwa namba wani Afrika mwaka 2004, 2008, 2013 na 2015, imeungana na Japan (wenyeji), Fiji, Marekani, New Zealand na Afrika Kusini (nambari nne za kwanza kutoka Raga ya Dunia ya msimu 2018-2019) na mabingwa Argentina (Amerika Kusini), Canada (Amerika Kaskazini), Uingereza (Ulaya) na Australia (Oceania) katika Olimpiki 2020 itakayofanyika jijini Tokyo.
Washindi wa Afrika mwaka 2016 na 2017 Uganda, ambao wanaongozwa na Mkenya Tolbert Onyango, na wafalme wa Afrika mwaka 2000, 2012 na 2018 Zimbabwe wamefuzu kushiriki mchujo wa mwisho wa kuingia Olimpiki utakaokutanisha mataifa 12 mnamo Juni 20-21 mwaka ujao.
Timu zingine zilizoingia mchujo huo wa mwisho ni Brazil na Chile kutoka Amerika Kusini, Jamaica na Mexico (Amerika Kaskazini), Ufaransa na Ireland (Ulaya), na Samoa na Tonga (Oceania). Mabingwa wa Bara Asia hapo Novemba 23-24 watajikatia tiketi ya moja kwa moja kushiriki Olimpiki nao nambari mbili na tatu waingie mchujo wa mwisho wa dunia.
Matokeo ya Kenya: Mechi ya kufuzu kuingia makundi – Kenya 36-7 Ivory Coast; Mechi za Kundi B – Kenya 50-0 Senegal, Kenya 33-0 Namibia, Kenya 24-7 Uganda; Nusu-fainali – Kenya 40-14 Madagascar; Fainali – Kenya 33-0 Uganda.
Matokeo ya Kombe la Afrika 2019 (Novemba 9):
Fainali – Kenya 33-0 Uganda;
Mechi ya kutafuta nambari tatu na nne – Zimbabwe 24-7 Madagascar;
Mechi ya kujaza nambari tano na sita – Namibia Namibia 28-5 Zambia;
Mechi ya kutafuta nambari saba na nane – Senegal 14-12 Nigeria;
Mechi ya kupata nambari tisa na 10 – Ghana 33-10 Morocco;
Mechi ya kutafuta nambari 11 na 12 – Tunisia 19-14 Ivory Coast;
Mechi ya kutafuta nambari 13 na 14 – Mauritius 31-0 Botswana.